CONAKRY,GUINEA

UONGOZI wa kijeshi nchini Guinea umesema wajumbe wa Baraza la Taifa la Mpito hawawezi kushiriki katika uchaguzi wa taifa na serikali za mitaa.

Jeshi hilo pia limesema litakubaliana kuhusu muda wa kuwepo kipindi cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi na baraza hilo litakuwa na wajumbe 81.

Kwa muda wa wiki mbili zilizopita uongozi wa kijeshi umekuwa ukifanya mazungumzo na viongozi wa umma na wafanyabiashara kuainisha mfumo wa serikali ya mpito.

Kulingana na hati ya mabadiliko, Kanali Mamady Doumbouya kiongozi wa mapinduzi ya Septemba 5, atakuwa rais, huku serikali ikimjumuisha waziri mkuu na baraza la mawaziri la kiraia.

Baraza hilo linatakiwa liwe na silimia 30 ya wanawake na litamjumuisha rais na makamu wawili wa rais ambao pia hawatoruhusiwa kugombea katika uchaguzi ujao.