KIGALI, RWANDA

SERIKALI ya Rwanda imetangaza kuwa, imepoteza askari wake wanne waliouawa katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Taarifa ya kuuawa wanajeshi wanne wa Rwanda nchini Msumbiji ilithibitishwa na msemaji wa jeshi la Rwanda katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rwanda kutangaza habari kuhusu kuuawa kwa wanajeshi wake ambao kwa ushirikiano na jeshi la Msumbiji wamekwisha likomboa jimbo la Cabo Delgado nchini humo ndani ya kipindi cha miezi miwili na nusu iliyopita.

Taarifa zaidi zinasema, idadi kubwa ya magaidi imeendelea kuuawa na baadhi kukamatwa huku wananchi waliokuwa wamekimbia makaazi yao katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Cabo Delgado wakiendelea kurejea katika maeneo yao.

Wanajeshi wa Rwanda wamekuwa wakishirikiana na wenzao wa Msumbiji tangu mwezi Julai, kwa ajili ya kurejesha udhibiti wa maeneo yaliyotawaliwa na wanamgambo wanaobeba silaha wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh.

Hatua ya askari hao wa Rwanda kutumwa Cabo Delgado inafuatia mapatano ya pande mbili wakati wa ziara ya Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi nchini Rwanda Aprili mwaka huu.

Machi mwaka huu,magaidi nchini Msumbiji waliuteka mji wa Palma wa kaskazini mwa nchi hiyo ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania, na kuua makumi ya watu na kuwalazimisha kuwa wakimbizi watu wengine zaidi ya 50,000.Eneo hilo limekumbwa na uasi baada ya kuanza mradi wa gesi wa dola bilioni 20.