NA TATU MAKAME

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema umefika wakati kwa serikali kuwashajihisha wananchi kufuatilia taarifa za mabadiliko ya tabia nchi ili kukabiliana na athari zake lakini pia kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya dunia.

Dk. Mkuya alieleza hayo hivi karibuni alipokuwa akifunga mkutano wa wadau wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, uliofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort.

Mkutano huo uliokuwa ukijadili masuala ya utumiaji wa vifaa vya kisasa kwenye uvuvi wa bahari kuu, Dk. Mkuya alisema wananchi wanapaswa kushajihishwa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi katika suala zima la ukuaji wa uchumi kupitia bahari kwa maendeleo ya nchi.

Aidha alisema kufanyika kwa mkutano huo kumetoa fursa kwa Zanzibar kuwa na taarifa kamili ya mabadiliko ya dunia na upatikanaji wa data kamili za mabadiliko ya tabia nchi duniani.

“Kufanyika kwa mkutano huu kunatoa fursa ya kujadili namna ya kutumia teknolojia kukusanya data za mabadiliko ya tabia nchi ili kutumia raslimali za bahari na kuweka mikakati bora kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya nchi,” alisema Dk. Mkuya.

Mkurugenzi Idara ya uratibu na maendeleo ya uchumi wa buluu na uvuvi, Kepteni Hamadi Bakari Hamadi, alisema mradi huo utaisaidia Zanzibar kutambua fursa za uvuvi kwa kutumia vifaa vya kisasa na kuondosha usumbufu kwa wavuvi.

“Wavuvi watakapotumia vifaa hivyo watajua sehemu gani kuna samaki na kwenda kuvua kwa njia rahisi bila kutumia muda mrefu kutafuta maeneo ya kuvua,” alisema Bakar.

Aliongeza kuwa kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuonesha ni vipi Zanzibar inaweza kutumia teknolojia ya kisasa (satellite) kudhibiti maeneo ya bahari na nchi kavu kwenye masuala ya uvuvi.

“Ikiwa mvuvi atamwaga mafuta baharini na mambo mengine yanayoharibu mazingira pia ataonekana kupitia satellite, teknolojia ambayo tunaamini kuongeza tija kwenye utekelezaji wa dhana ya uchumi wa buluu,” alisema.