ZASPOTI
SERIKALI imeshauriwa kuziunga mkono timu za soka za wanawake kwa kuzitafutia wadhamini ili ziweze kufanya vyema katika mashindano mbali mbali na kuitangaza vyema nchi.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya wachezaji wa mchezo huo wa timu mbali mbali za wanawake wakati walipozungumza na Zaspoti kwa nyakati tofauti.
Wachezaji hao, walisema, wamekua na wakati mgumu na wengine kulazimika kushindwa njiani na kuachana na soka kutokana na hali ngumu wanazokua nazo.

Walisema wamekua wakijitahidi katika kucheza soka lakini tatizo kubwa linalowakabili ni gharama ambazo zinawafanya washindwe kufikia malengo.
“Naiomba serikali yetu itusaidie na sisi tunaocheza soka la wanawake kwa kututafutia wadhamini ili tuweze kufika mbali.

“Hali zetu za maisha ni ngumu na tunataka tuwe kama wenzetu, lakini, hali haziruhusu”, alisema, Mwanajuma Haji mchezaji wa New Generation.
Alisema, sababu za kutolewa mapema katika michuano ya kuwania Kombe la Wanawake Afrika Mashariki nchini Kenya kulisababishwa na kukosa maandalizi mazuri na ya mapema tofauti na wenzao.

Naye, Khadija Omar, mchezaji wa timu ya Chwaka Stars, alisema, kukosekana kwa udhamini katika soka la wanawake ni miongoni mwa sababu zinazochangia kushuka kwa soka hilo nchini.
Aidha, alisema, jamii ya Kizanzibari imelipokea soka la wanawake kwa mtazamo mbaya hali inayopelekea kutofikia malengo kama zilivyo nchi nyengine.

“Wenzetu Tanzania Bara timu zao ziko mbali, wanacheza mpira mzuri na wanazitangaza timu zao, lakini, dhana potofu ndio zinazoharibu tusicheze soka Zanzibar”, alisema.
Nae Fayza Hassan, mchezaji wa Zanzibar Queen, aliwaomba wazazi na wananchi mbali mbali kuachana na dhana potovu na kuwaunga mkono wachezaji hao kwani kushiriki katika mchezo huo ni kujikwamua na tatizo la ajira.