KABUL, AFGHANISTAN

WANAWAKE nchini Afghanistan wameandamana, wakidai haki za kupata elimu na kazi wakati Taliban ikifanya maandalizi ya kuunda serikali mpya.

Makumi ya wanawake walishiriki maandamano hayo katika mji mkuu wa Kabul,wakipiga kelele kwamba serikali ambayo hailindi haki za wanawake inakosa uhalali.

Wakiwa wamebeba mabango yaliyosomeka kwamba hawaogopi,wanawake hao waliwaasa Taliban kutoharibu haki zao za elimu na ajira.

Baadhi ya wanawake walilalamikia kuwa walipigwa na wapiganaji hao wakati wa mapambano kati ya waandamanaji na wapiganaji wa Taliban wenye silaha.

Mwanamke mmoja alisema alishiriki kwa sababu alitaka kuwasilisha ujumbe kwa Taliban, sauti za wanawake ambao hawawezi kwenda kazini ama skuli.

Taliban ipo katika majadiliano na makundi mengine nchini humo ili kutangaza kuanzishwa kwa serikali mpya.

Wajumbe waandamizi wa kundi la Taliban walisema kwamba haki za wanawake zitaheshimiwa ndani ya ukomo wa sheria ya Kiislamu.