KIGALI, RWANDA

WANAWAKE wamehimizwa kushiriki katika uchaguzi wa ndani ambao umepangwa kufanyika Oktoba, kwa kutoa mgombea wao na kujitokeza kupiga kura.

Wito huo ulitolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Baraza la Kitaifa la Wanawake.Mkutano uliwaleta pamoja wawakilishi wa wanawake kutoka wilaya zote kujadili maswala ya kijinsia nchini.

Immaculee Mukarurangwa, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi, alisema kulikuwa na pengo kubwa la wanawake katika uongozi wa mitaa.

“Tuna viongozi wengi wa wanawake lakini wanashikilia nyadhifa za juu kama vile katika bunge, lakini chini ya ngazi ya serikali za mitaa bado kuna pengo la viongozi wanawake,” Mukarurangwa alisema, akitaka uhamasishaji wa wanawake kote nchini na kuwapa nguvu kushiriki uchaguzi ujao.

Jeannette Bayisenge, Waziri wa Jinsia na Ukuzaji wa Familia, alisema katika uchaguzi uliopita wa asilimia 32.2 ya viongozi waliochaguliwa walikuwa wanawake.

Alisema wanahitaji kuongeza juhudi mara mbili na kuhakikisha wanawake wengi wanapigiwa kura, haswa wasichana wadogo ambao wanapaswa kuhamasishwa kuhusu uchaguzi huo.

Alisema wanawake wanaochaguliwa katika ngazi hiyo ya mitaa watasaidia kutatua maswala muhimu kama mimba za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia, na visa vya unajisi, kwa sababu wanawake waliopigiwa kura watasaidia kutatua shida hizo mapema lakini pia watatoa ushauri, na msaada zaidi kwa wasichana wadogo na kuhakikisha hawaachwi nyuma.

Jackline Kamanzi, Katibu Mtendaji Baraza la Kitaifa la Wanawake alisema kwamba baraza litaimarisha juhudi zake za uhamasishaji, haswa katika kuvutia wagombea wanawake wenye ulemavu na wasichana wazima.

Alisema watahakikisha kampeni hizo ambazo ziliingiliwa na Covid-19 zinaendeshwa kote nchini katika hatua zote na kuhakikisha kuwa zinahusisha wengi kadiri wawezavyo.

Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi, kuna viti 340,000 katika uongozi wa mitaa ambavyo vitapokea viongozi wapya.