NA MWAJUMA JUMA

UMOJA na mshikamano ndio silaha kuu katika maendeleo ya nchi yoyote duniani na kama zilivyo nchi nyengine Zanzibar ni moja ya nchi ya mfano kwa kuongoza kwa amani na utulivu.

Hali hii inatokana na uthubutu wa viongozi wetu ambao kwa pamoja waliungana na kufanya maridhiano yaliyofikia uamuzi wa kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo mpaka sasa tunaona faida yake ikiwemo kuwaunganisha wananchi.

Katika hali ya kawaida jambo hili kubwa la kisiasa wapo baadhi ya wananchi wachache pengine wasingependa kufikiwa maridhiano ambayo yatawaunganisha wananchi kwa sababu kila zipotokea hitiliafu pengine kwao huwa kuna faida.

Aidha katika suala zima la maridhiano hili sio tu kwa viongozi bali kila mmoja wetu anapaswa kuunga mkono juhudi za viongozi. Tukumbuke kwamba Zanzibar imetoka katika wakati mgumu wa siasa ambapo tusingependa zitokee tena.

Katika miaka ya nyuma watu walifikia kukwazana na wapo ambao waligawana ukoo ilimradi tu kwa sababu za kisiasa, lakini sasa tumekuwa kitu kimoja na tutakiwa tuendeleze ili kuijenga nchi yetu kwa pamoja.

Tumpongeze sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye amekuwa muhimili wa kuwaunganisha wananchi kwa kile anachoamini kuwa bila ya umoja na mshikamano wa wanahi hakuna maendeleo.

Kama viongozi wetu wa pande zote kuu za kisiasa hapa Zanzibar wameungana na kuendesha nchi kwa pamoja kuna umuhumi kwetu sisi kuendelea kuunga mkono maridhiano ya serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuwa kufanya hivyo ndio kupigania maslahi ya Zanzibar.

Moja ya faida kubwa ya maridhiano ambayo wananchi wananufaka nayo hivi sasa ni hatua ya kuondosha chuki, misimamo mikali ya kisiasa ambayo wakati mwengine ilifikia hatua ya kutishia amani.

Kuunga mkono serikali ya Umoja wa kitaifa kwa kila Mzanzibari ni jambo muhimu katika kusaidia kuacha urathi mzuri wa mshikamano na amani ya kweli, kwa kizazi cha sasa na kijacho na kuifanya nchi kuwa imara zaidi kimshikamano.

Kuwepo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa kumezingatia na kujali maslahi ya wananchi na dhamira ya kuwapatia maendeleo makubwa, hivi tumeona wapi nchi ambayo wananchi wanazozana wenyewe kwa wenyewe ikapata maendeleo.

Hivyo wananchi kwa jumla, wa Unguja na Pemba na popote walipo Wazanzibari kuendelea kushikamana kwa kuendelea kufanya juhudi za kujenga misingi bora na imara ya kuendeleza serikali hiyo.