NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali, amesema sekta ya usafirishaji kwa njia ya bahari ni ya kimataifa hivyo inahitaji ushirikiano, ili kuona bidhaa na huduma zinazosafirishwa zinaondokana na vikwazo.

Akifungua warsha ya siku mbili ya uhamasishaji wa wenye mzigo huko Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Malindi Mjini Unguja.

Waziri Rahma alisema, ili kufikia lengo hilo kunahitajika majadiliano juu ya kutafuta njia bora za kuimarisha sekta hiyo kulingana na wakati.

Alisema ni vyema kupitia taasisi za usafirishaji za serikali na binafsi kuyaelewa matatizo yanayowakabili wamiliki wa mizigo, kwa lengo la kutafuta suluhisho na kuwa mstari wa mbele kutetea na kuelimisha wasafirishaji juu ya mbinu bora za kushiriki biashara za kimataifa.

Aidha alisema, wasafirishaji wa Zanzibar ni njia ya kushirikiana na wasafirishaji wengine katika kanda na duniani  kote na kuwa katika nafasi nzuri ya kuvutia msaada wa wafadhili kwa mipango mbalimbali ambayo sekta hiyo inahitajika kutekeleza.

Hivyo, aliwaomba wadau wa Zanzibar kuunga mkono mpango huo ili isibaki nyuma katika kile kinachoonekana kwani zoezi la kikanda na kimataifa.

“Kabla ya yote, niwapongeze ISCOS ka majukumu wanayofanya katika kulinda maslahi ya nchi wanachama kwa kuwahamasisha waagizaji na wauzaji wetu wa nje juu ya masuala yanayojitokeza katika sekta hii pamoja na kuzishauri serikali zetu juu ya sera zinazofaa kwa ssekta ya usafirishaji wa baharini” alisema.