Accra, GHANA

NCHI za Kiafrika zimerikodi maambukizi mapya 25,477 ya COVID-19 katika masaa 24 hadi Jumamosi na hivyo kuifanya jumla ya watu walioambukizwa ugonjwa huo hadi sasa barani humo kuwa milioni 7.87.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa cha Afrika, watu wasiopungua 601 walipoteza maisha kwa sababu zinazohusiana na COVID-19 katika masaa 24 hadi Jumamosi na kusababisha vifo vilivyotokana na ugonjwa huo barani humo kuwa 198,587.

Idadi ya waliopona COVID-19 hadi sasa ni zaidi ya milioni saba.

Kati ya maeneo matano ya kijiografia katika bara hilo, eneo la Kusini mwa Afrika lina kesi nyingi zaidi za COVID-19 ambazo zimefika milioni 3.7 ikifuatiwa na Kaskazini ambako maambukizi yamefika milioni 2.4 huku ukanda wa Afrika Mashariki ukiwa na kesi 918,400, Afrika Magharibi 610,100 na Afrika ya Kati 221,500.

Dozi milioni 137.7 za chanjo zilisambazwa hadi sasa kwa ajili ya matumizi katika bara la Afrika lenye wakaazi bilioni 1.3, ambapo dozi milioni 104.2 zishatolewa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa nchi 42 kati ya 54 za Afrika hazitoweza kuwachanja watu walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa corona.

WHO ilisema uhaba wa chanjo barani Afrika unatokana na nchi tajiri kuendelea kuhodhi chanjo ya virusi vya corona.