PYINMANA, MYANMAR

WATU kutoka nchini Myanmar wameandamana duniani kote na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya utawala wa jeshi nchini mwao, kabla ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN unaotarajiwa kuanza leo.

Maandamano yalifanyika katika nchi zaidi ya kumi mwishoni mwa wiki iliyopita.Waandamanaji wanaitaka jumuiya ya kimataifa kukataa utawala wa jeshi na kuitambua Serikali ya Umoja wa Taifa, NUG.

NUG inaundwa na makundi yanayopigania demokrasia na inamuunga mkono kiongozi mkuu wa nchi hiyo aliyeng’olewa madarakani Aung San Suu Kyi.

Jeshi lilitwaa madaraka kupitia mapinduzi mwezi Februari.Unyanyasaji wa wapinzani uliendelea kote nchini humo kwa kipindi cha miezi nane iliyopita.

Kundi moja la kutetea haki za binadamu linasema raia zaidi ya 1,000 waliuawa wakiwemo watoto, watu zaidi ya 8,000 walikamatwa.Watu wapatao 1,400 walijumuika na maadamano hayo jijini Tokyo.

Walipaza sauti wakisema ‘ifanye Myanmar kuwa huru,’ na kupiga saluti ya vidole vitatu inayohusishwa na maandamano ya kupinga utawala wa jeshi.