NA ASYA HASSAN
JUMUIA ya Kwarara Development Organazation, imeahidi kushirikiana na serikali, ili kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenyemahitaji maalum.
Katibu wa Jumuia hiyo, Suleiman Vuai Suleiman, alisema hayo katika skuli ya Makadara alipokuwa akizungumza na baadhi ya vijana wanaotumia dawa za kulevya.
Alisema taasisi binafsi zinamchango mkubwa wa kusaidia maendeleo ya nchi, hivyo ili kufanikisha hilo serikali inapaswa kuendeleza kushirikiana nazo hatimae malengo ya kuanzishwa kwake yaweze kufikiwa.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuwafanya watu hao kujitambua pamoja na kufahamu fursa mbalimbali ziliyopo nchini, ili waweze kuzipata kama walivyo watu wengine.
Katibu huyo alifahisha kwamba lengo la jumuiya hiyo ni kuwasaidia watu hao kuweza kuacha matumizi ya dawa za kulevya na kupata fursa ya kujumuika na wenzao katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Alifahamisha kwamba vijana ndio nguvu kazi ya taifa, hivyo wanahitaji kuwekewa mazingira na mifumo imara, ili waweze kunufaika na rasilimali mbalimbali ziliyopo nchini.
Sambamba na hayo alifahamisha kwamba watu hao ni wadau muhimu na wananchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya nchi yao kupitia Nyanja mbalimbali.
“Jumuia tumedhamiria kuwasaidia watu hawa ili waweze kupata fursa ya kuzitumia rasilimali mbalimbali ziliyopo nchini na waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na waweze kujitegemea wenyewe,”alisema.