NA LUTFIA CHUM (MUM)
Wafanyabiashara wa Ukindu katika maeneo ya Saateni Mkoa wa Mji Magharibi Unguja, wameiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma katika biashara ya ukindu, kwa kuwapatia masoko, ili kuweza kuondokana na changamoto zinazowakabili kwa mda mrefu sasa.
Wakizungumza na Zanzibar Leo, wamesema , wengi wao hawana misingi mizuri ya kuendesha biashara hiyo, kufanya hivyo kutasaidia na kuboresha mazingira wanayofanyia kazi kila siku, ili kujiinuwa kimaisha .
Wafanyabiashara hao wamesema, biashara ya ukindu kwa sasa ni ngumu, kwani hakuna wanunuzi wa uhakika , hali inayopelekea kukaa kutwa nzima bila kuuza, jambo ambalo linaogeza ugumu wa maisha.
Wamesema kuwa, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika biashara ya ukindu, kwani mazingira wanayo fanyiabiashara ni changamoto pia, ingawa wapo katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20 sasa, lakini bado mazingira hayajawa rafiki kwao.
Wakizungumzia kwa upande wa ushuru wamesema, kila wiki wanalipa elfu saba kwa ajili ya usafi, lakini ni jambo la kushangaza hakuna usafi unaofanywa hali inayowalazimu kufanya wao wenyewe, ili kuona mazingira yanayowazunguka yanakuwa katika usafi.
Wafanya biashara hao, wameiomba serikali, kwa kuwatafutia masoko ya ndani na nje ya Zanzibar, kwani kufanya hiyo kutainua biashara ya ukindu hapa Zanzibar, na kupelekea kuongezeka kwa mapato serikalini pia kwa mtu mmoja mmoja.
Aidha wafanya biashara hao wamesema ni vyema serikali kuwapatia mikopo , kwa lengo la kukuza mitaji yao, ili kuboresha zaidi, ambayo bado haijawa ya uhakika.
Ofisa Uhusiano wa Baraza la Manispaa Mkoa wa Mjini, Magharib Seif Ali Seif, amesema muongozo wa serikali ni kulipa kila mwezi na siyo kila wiki kwani Kaya , Maduka , Magodauni na Stoo vyote vinatozwa kwa mwezi na hakuna malipo ya usafi yanayofanywa kwa kila wiki.