Kuanza kutumia ‘tablets’ kwenye vikao

NA ALI KINASA, MUZNAT HAJI (SCCM)

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wapatiwa vifaa vya ‘tablets’ pamoja na mafunzo kwa ajili ya matumizi ya vifaa vya eletroniki, ikiwa ni hatua itayowafanya kukuza matumizi ya TEHAMA katika shughuli zao.

Kaimu Mkuu wa Utawala Ofisi ya Baraza la Wawakilishi, Abdalla Ali Shauri, amesema jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo, huko Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema tayari wameanza kutoa mafunzo hayo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, linalowataka wajumbe wa Baraza hilo kutumia mifumo ya kisasa katika uendeshaji wa shughuli zao.

Alisema hatua hiyo ina dhamira ya kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za baraza hilo kwa kuondoa matumizi ya fedha kwa ajili ya kununulia karatasi na badala yake watatumia teknologia hiyo ya ‘tablets’.

“Kawaida tunakua tunatumia karatasi ambazo hizi zinahitaji kuchapishwa, lakini kuanzishwa kwa mfumo huu wa kilektroniki, utawawezesha wajumbe wote kutumia ‘tablets’ ambazo zitakua zimeingizwa taarifa zote zinazohitajika kutumika kwa ajili ya baraza, hivyo gharama za machapisho hazitakuwepo” alisema Kaimu Mkuu huyo.

Alisema matumizi ya karatasi ndani ya Baraza hilo hivi sasa ni makubwa yanayoligharimu fedha nyingi, jambo ambalo litaondoka ikiwa wataanza kutumia mfumo huo, kwani lengo lengo ni kuleta matokeo chanya katika shughuli za Baraza.

Aidha, alisema mfumo huo hautaishia katika Baraza la kumi bali utakua ni endelevu kwa mabaraza yajayo, kwani lengo ni wa kudumu katika mfumo huo, kama  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linavyofanya  katika kuendesha shughuli zake kwa kutumia TEHAMA.

“Tablets tayari tumezigawa kwa kila mjumbe ambapo zitakusanya taarifa na hizi zitatumika makhsusi kwa ajili ya shughuli za baraza tu, ili kurahisisha kazi” Kaimu Mkuu wa Utawala alisema.