NA MARYAM HASSAN

KITENGO cha kupambana na dawa za kulevya kimewatia mbaroni vijana wawili wakiwa na majani makavu yanayodhaniwa kuwa ni bangi.

Vijana hao walikamatwa maeneo ya Kikwajuni, wilaya ya Mjini na mkoa wa Mjini Magharibi, wakakati askari wa kitengo hicho waiwa katika msako wa kuwakamata watu ambao bado wanendeleza uhalifu wa kutumia dawa hizo.

Mkuu wa kitengo hicho Mrakibu wa Polisi, Omar Khamis alieleza hayo wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Kilimani, Unguja na kuongeza kuwa vijana hao walikamatwa Septemba 20, mwaka huu saa 7.00 za mchana katika maeneo ya Kikwajuni, Zanzibar.

Alieleza kuwa Sajenti E. 2234 Ali, akiongoza wenzake walifanikiwa kumkamata Issa Ramadhan Soud (20) mkaazi wa Kikwajuni akiwa na nyongo 28 za majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa gramu14.

Aidha alisema kwamba siku hiyo hiyo alikamatwa Ali Abdalla Ali (21) akiwa na kifurushi cha majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa gramu 95.

Alisema upelelezi wa shauri hilo ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Mmoja wa askari hao alisema zoezi la ukamataji watuhumiwa muda mwengine linakuwa gumu kwa sababu baadhi ya wananchi hawataki kutoa ushirikiano.

“Sisi tunafika eneo la tukio lakini tukiwahoji wananchi wanasema hawajui aidha nyumba inayouzwa au eneo linalofanyika vitendo hivyo, hivi wakiendelea kuficha je lengo litafikiwa kutokomeza biashara hii haramu,” alisema Sajenti E E. 2234 Ali.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa Zanzibar hakuna tena uuzwaji wa biadhara hii haramu ya dawa za kuevya.

Hivyo aliitaka jamii kuendelea kutoa mashirikiano pindi askari watapofika katika maeneo yao kwa ajili ya kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote ambao watakutwa na hatia hizo.