NA MADINA ISSA

OFISA Kazi kutoka Ofisi ya Raisi, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, kupitia Idara ya Ajira, Kassim Maulid Juma, amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa za ajira zinapotokezea ili kuendeleza shughuli za kukuza uchumi nchini.

Akizungumza baada ya kuwapatia mafunzo vijana wanaotaka kwenda Dubai kwa ajili ya ajira, alisema wizara inafanya kazi ya kuwaunganisha vijana katika kuwapatia ajira ,hivyo ni vyema kuzitumia ipasavyo nafasi hizo, ili lengo lililokusudiwa lliweze kufikiwa.

Alisema nafasi mbali mbali za ajira zinapotokezea vijana wanashindana kuzitumia kutokana na ukosefu wa elimu pamoja uwelewa mdogo juu ya nafasi hizo za kazi za nje ya nchi.

Aidha alifahamisha kuwa Wizara kwa kushirikiana na kampuni ya uwakala binafsi wa ajira Zanzibar DXB Company LTD, inachukuwa jitihada za kusimamia vijana wanapokwenda nje ya nchi kufanya kazi, ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira salama.

Nae Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala Binafsi wa Ajira Zanzibar, Jafar Hussein Babbu, aliwataka vijana hao kuwa waadilifu na waaminifu katika utekelezaji wa kazi zao, ili waweze kutumiza malengo yao waliyojiwekea.

Nao vijana waliopatiwa mafunzo hayo, waliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia nafasi ya kwenda kufanya kazi katika hali ya usalama.

Hivyo, waliahidi kuyatumia mafunzo waliyopatiwa katika ufanyaji wao wa kazi, ili kuweza kufikia malengo waliyoyakusudia.