ZASPOTI

SERIKALI iliridhia Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF) kuwa na ngazi za mikoa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuendana na mfumo wa Tanzania Bara ili misaada itakayotokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na FIFA iwe inaendana na mfumo wa nchi nzima.
Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, aliyasema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said.

Mwakilishi huyo alitaka kujua katiba ya ZFF haiwezi kufanya kazi hadi ipitiwe na kuridhiwa na Msajili wa Vyama vya Michezo, Je, ni sababu zipi zilizopelekea serikali kukubali kurejeshwa kwa ngazi hiyo ya mkoa.
Alisema, kugatua soka ili ofisi za wakuu wa Mikoa ambao wana dhamana na kusimamia maendeleo ya jumla katika mikoa wawe na programu maalumu za kukuza na kuendeleza klabu katika mikoa yao ikiwemo kupanga miundombinu, kuandaa mashindano na usimamizi mzuri wa mpira wa miguu.

Aidha, alisema, vyama vya mikoa ndiyo vyenye mamlaka ya kikatiba ya kusimamia vyama vya wilaya kwa lengo la kutanua wigo wa mashindano na kuongeza hamasa na vuguvugu la mpira kwa kila mkoa na hivyo baadae kuwa na timu zenye ushindani wa kweli.
Waziri Tabia alibainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba za Vyama vya Mpira vya Mikoa, vyanzo vya fedha ambavyo vinategemewa na ofisi za ZFF Mkoa ni pamoja na ada ya uanachama, ada ya ushiriki wa mashindano kwa kila klabu, mauzo ya fomu za usajili na uhamisho wa wachezaji,
mapato yanayopatikana kutokana na faini zinazotolewa kwa klabu iliyoadhibiwa kisheria na asilimia ya mapato yanayopatikana kutokana na viingilio vya uwanjani katika mashindano ya ligi ya Mkoa.

Akizungumzia ufufuaji wa mashindano ya ngalawa, suala lililoulizwa na Mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe, aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kuendeleza utamaduni wetu kwa kuyafufua na kuyaimarisha mashindano hayo, alisema, bado yapo na wizara inaendelea kuyaendeleza kama moja ya tunu ya urithi wa utamaduni asili wa wananchi wa Unguja na Pemba.
Alisema, mashindano hayo yamekua ni moja ya kivutio muhimu katika maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi, maadhimisho ya Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari, lakini, pia kupitia Tamasha la Utalii linaloitwa Rafiki Network ambapo hufanyika Pemba.

Alisema matamasha yote hayo yanalenga kuutumia utamaduni kama moja ya kivutio cha kuitangaza Zanzibar huku tukiendeleza haiba ya urithi wa utamaduni.
Hata hivyo, alibainisha mara ya mwisho mwaka 2018 mashindano hayo yalifanyika Pemba katika wilaya ya Mkoani na Kizimkazi Unguja.
Kwa mwaka 2020, Waziri Tabia alisema mashindano hayo yaliahirishwa kutokana na msiba wa kitaifa.