NA SABIHA KEIS, WAMM

IMEELEZWA kuwa ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko hususani katika tasnia ya uhusiano na habari katika taasisi za serikali ni lazima watendaji kufanya kazi kwa bidii na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pembe Juma, aliyaeleza hayo huko ofisini kwake Maisara katika kikao cha pamoja baina yake na watendaji wa kitengo cha Uhusiano na Habari cha wizara hiyo kwa lengo la kujadili maendeleo ya utekelezaji wa majukumu yao na kuleta mafanikio.

Alieleza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na ubunifu katika majukumu yao ya kila siku jambo ambalo litakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko na kuifanya wizara  kuweza kufikia malengo yake iliyojipangia.

“Ili kukuza ufanisi kwenye kazi ni lazima tuwe wabunifu na tuwe tayari kubadilika ndani ya taasisi ili tuweze kutoa huduma bora kwa wananchi lakini pia kuongeza tija,” alieleza waziri Pembe.

Alifahamisha kuwa ili taasisi isonge mbele ni lazima kwa watendaji kufanya kazi kwa ushrikiano,biidii na kujituma kwa kufuata kanuni ya utumishi wa umma kama inavyoelekeza.

Aidha Riziki alisisitiza haja ya watendaji hao kuwa na mpango kazi mzuri katika utekelezaji wa majukumu jambo litakalowasaidia kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji wa hali juu katika taasisi.

Aidha aliwataka watendaji hao kujiongezea kielimu jambo ambalo litapelekea kuleta mafanikio chanya katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku na kujiongezea umahiri mkubwa kiutendaji.

“ili twende sambamba na kasi ya utendaji katika majukumu yetu ni wajibu kwa kila mtumishi kujiongeza kielimu  na kuongeza ubunifu kazini,” alisisitiza.

Wakizungumza katika kikao hicho, baadhi ya wafanyakazi wa kitendo cha hicho, waliamuahidi Waziri huyo kuyafanyia kazi maelekezo aliyowapatia sambamba na kuomba kuwekewa mazingira mazuri yakiwemo ya vifaa na eneo la kufanyia kazi.

Walisema kitengo hicho ni muhimu katika kukuza mahusiano kati ya wizara hiyo, watendaji wake na wadau wengine wakiwemo wananchi hivyo kikijengewa uwezo na kuwezeshwa kufanya kazi zake kikamilifu tija itapatikana.