NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita ametoa mkono wa pole kwa bodi na menejimenti ya Shirika la Magazeti ya Serikali, kufuatia kifo cha Khamis Amani Suweid aliyekuwa mfanyakazi wa shirika hilo.

Khamis Amani (49), alifariki usiku wa kuamkia jana nyumbani kwao mtaa wa Kwahani mjini Zanzibar na kuzikwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi ‘B’ baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Waziri huyo alisema kufuatia kifo cha mfanyakazi huyo wa Shirika la Magazeti ya Serikali anatoa mkono wa pole na kukielezea kifo hicho kuwa ni pigo kutokana na mchango wake katika utendaji wa kazi za kila siku.

“Nitoe pole kwa bodi na menejimenti ya Shirika la Magazeti kwa kifo cha mtumishi wa shirika hilo, pia pole kwa wanafamilia ambao wamempoteza mpendwa wao”, alisema waziri huyo ambaye alihudhuria mazishi hayo.

Hapo jana waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hapa Zanzibar walishiriki kwenye mazishi hayo yaliyofanyika katika mtaa wa Kwahani na kuzikwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe.

Akizungumza na Zanzibarleo, Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti, Yussuf Khamis Yussuf alisema Khamis Amani aliugua kwa muda mfupi na siku mbili zilizopita hali yake ilizorota kabla ya kufikwa na mauti usiku wa kuamkia jana.

Alisema Shirika limempoteza mfanyakazi mahiri mwenye kupenda kuwajibika, hata hivyo kifo chake ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Mhariri huyo alitoa salamu za pole kwa wanafamilia ndugu na jamaa kwa kumpoteza mpenda wao huyo aliyekuwa nguzo katika familia.

Khamis Amani Suweid alizaliwa Oktoba 25 mwaka 1973 katika mtaa wa Kwahani ambapo aliajiriwa Oktoba 1 mwaka 2014.

Alipata mafunzo ya uandishi wa habari kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Idara ya Habari Maelezo Julai 2001 hadi Julai 2002, ambapo hadi anafariki alikuwa mhariri msaidizi.