NA AMEIR KHALID

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Khamis Juma amesema Wizara ya Elimu itaendelea kusimamia michezo ili kukuza vipaji kwa wanafunzi.

Alitoa kauli hiyo wakati akifungua kongamano la michezo katika skuli, kwa  wadau mbalimbali wa michezo ukumbi wa Sanaa Rahaleo.

Alisema michezo ni akili hivyo mwanafunzi kushiriki katika michezo humsaidia sana kuepukana na vitendo viovu  pamoja na kuchangia kukua vyema kiakili pamoja na afya yake.

Alisema  itahakikisha michezo inarudi katika hadhi yake hasa katika skuli, hivyo kuna umuhimu kwa wadau hao kutoa michango yao ili kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Alisema bado Zanzibar inahitaji mabalozi wa michezo kwenye Mataifa mbali mbali Duniani, hivyo ni vyema kushirikiana kuwajenga mabalozi hao kupitia  skuli, ambapo hadi sasa haijatangazwa vyema.

Aidha amekiri kuwepo kwa matatizo mbalimbali ya kimichezo ndani ya wizara ambapo tayari ameweka muongozo ili uweze kujadiliwa ndani ya mkutano huo.

Hivyo alisema kongamano hilo litaisaidia sana wizara kupata muongozo mzuri wa kuimarisha michezo nchini.

Alisema muda umefika kwa kila mtu kujua nafasi yake na wajibu wake ili kuweka mikakati sahihi ya kuhakikisha Zanzibar inakua na vipaji mbalimbali vya michezo kupitia Skuli.