NA ASYA HASSAN

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA), imesema itaendelea kuwekeza kupitia sekta ya elimu ili kwenda sambamba na malengo ya serikali juu ya kutoa elimu bila malipo.

Waziri wa wizara hiyo Simai Mohammed Said alisema hayo alipokuwa akifungua maonesho ya kitaaluma ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kusheherekea miaka 57 ya elimu bila malipo Zanzibar.

Alisema wizara hiyo itaendelea kuongeza vifaa vya kufundishia katika skuli zote za Unguja na Pemba ili kuwafanya vijana waweze kujifunza kwa ufanisi na kuleta maendeleo ndani ya nchi yao.

Alifahamisha kwamba serikali imeweka sera, sheria juu ya suala hilo ili kuona kila mwananchi anapata haki hiyo bila ya ubaguzi.

Mbali na hayo alifahamisha kwamba wizara hiyo itazidi kuwaandaa vijana na kuviendeleza vipaji viliyopo ili kuhakikisha vinauzika katika soko la ajira liliyopo ndani na nje ya nchi.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa wataalamu wa ndani waliyobobea katika fani mbalimbali.

Akizungumzia maonesh hayo alisema yatasaidia kuwaelimisha jamii katika shughuli mbalimbali za kimaendele pamoja na kujifunza vitu mbalimbali kupitia mabanda hayo.

Hata hivyo alitumia fursa hiy kuiomba jamii na wanafunzi kutumia siku tatu hizo katika kupata elimu mbalimbali iliyopo katika mabanda hayo.

Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuwaomba walimu, wazazi na wadau wengine kutoka Nyanja mbalimbali kuzidi kushirikiana ili kupatikana maendeleo bora katika sekta hiyo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali Khamis alisema serikali itaendelea kutoa elimu bure ili kwenda sambamba na malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni, Sichana Haji Foum alisema lengo la maonesho hayo ni kuonesha vipaji na maendeleo mbali mbali yaliyopo katika sekta hiyo.