NA SABIHA KEIS, WAMM
KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Joseph Kilangi amesema kuwa wizara hiyo itaendelea kuyaendeleza na kuyathamini mazuri yote yaliyofanywa na viongozi waliotangulia.
Kilangi alieleza hayo ofisini kwake Maisara Mjini Zanzibar katika hafla ya kumuaga aliekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Ali Khalil Mirza aliemaliza muda wake wa utumishi.
Alisema kuwa si jambo baya kuiga mazuri yaliofanywa na waliostaafu, au waliomaliza muda wa utumishi serikalini kwani yalikuwa na lengo la kuleta maendeleo ya serikali, kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Kipindi cha miaka 30 ya utumishi wa umma si kipindi kidogo, hivyo tunapokuwa katika mazingira ya utumishi ni busara kufanyakazi kwa mashirikiano nidhamu, na uwajibikaji kufanya hivyo kutawezesha taasisi kufikia malengo iliyojipangia”, alisisitiza.
Aidha Kilangi alisisitiza haja kwa watumishi kuwa na tabia ya kupendana wenyewe na kuachana na tabia ya pelekeana majungu hususana wakati wanapokua kazini kwani kufanya hivyo kunarudisha nyuma ufanisi katika kazi.
Sambamba na hilo, Kilangi alisema kuwa kawaida mtumishi anapokua katika utumishi na kutenda mazuri kwa anaowatumikia basi mazuri hayo humrudia mwenyewe, hivyo ametumia nafasi hiyo kumpongeza alikuwa katibu mkuu huyo mstaafu kwa mazuri aliyoyaonesha na kuwataka wengine kuiga mfano wake.
Akitowa neno la shukurani, Mirza aliwataka wafanyakazi wa wizara ya Ardhi kufanya kazi kwa nidhamu umoja na mashirikiano na kuachana na tabia ya malumbano sehemu za kazi.
Aidha aliuhakikishia uongozi wa wizara ya Ardhi kuwa atashirikiana nao kwa kila hali pale atapohitajika kwa lengo la kuona kuwa wizara inafikia malengo yake iliyojiwekea.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenziwe, Kaimu Mkurugenzi Wakala wa Majengo, Kassim Ali Omar alimshukuru Ali Khaalil Mirza kwa mashirikiano katika kipindi chote cha utumishi wake kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wamemuahidi kuendeleza ushirikiano wao kwake.