UTARATIBU wetu wa maisha unazunguka saa 24 kwa siku na saa 12 za jua, na saa nyengine zilizobakia ni wakati wa usiku. Lakini, je! Ulijua kwamba kuna maeneo ulimwenguni ambapo jua halizami kwa kwa zaidi ya siku 70?

Fikiria jinsi inavyopendeza watalii kufuatilia muda, wakati hata wenyeji wenyewe wanachanganyikiwa kwa kuwa bila jua kwa siku 70 kufuatana. Ikiwa ungependa kujua zaidi, hapa kuna maeneo 6 duniani ambapo jua hukosa kutua.

Nchi ya Norway, iliyoko kwenye mzunguko wa Aktiki, na huitwa ‘Ardhi ya Jua la Usiku wa Manane,’ ambapo kuanzia Mei hadi mwishoni wa Julai, jua halizami kabisa.

Hii inamaanisha kuwa kwa karibu kipindi cha siku 76, jua huwa halizami. Katika eneo la Svalbard liliopo nchini humo jua linaangaza mfululizo kutoka Aprili 10 hadi Agosti 23.

Unaweza kupanga ziara yako mahali hapo wakati huo na kuishi kwa siku kadhaa, wakati kukiwa hakuna usiku.

Eneo jengine ni Nunavut liliopo nchini Canada ambalo lipo karibu digrii mbili juu ya mzunguko wa Aktiki, katika maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Canada.

Mahali hapa pana karibu miezi miwili ya jua kwa saa 24, huku wakati wa msimu wa baridi, mahali hapo huona karibu siku 30 mfululizo za giza kamili kukiwa hakuna mchana.

Iceland, ni kisiwa kikubwa zaidi barani Ulaya baada ya Uingereza na pia inajulikana kwa kuwa nchi ambayo haina mbu.

Wakati wa majira ya joto, usiku huwa uko wazi huko Iceland yaani hakuna giza, na wakati wa mwezi wa Juni, jua halizami kamwe.

Ili kuona jua la usiku wa manane katika ubora wake likiwa linang’aa, unaweza kutembelea jiji la Akureyri na kisiwa cha Grimsey kwenye mzingo wa Aktiki.

Eneo jengine ni Barrow liliopo katika jimbo la Alaska nchini Marekani, kuanzia mwishoni mwa Mei hadi mwishoni mwa Julai, jua halizami katika eneo hilo, ambalo baadaye hufidiwa kutoka mwanzoni mwa Novemba kwa siku 30 zijazo, ambapo jua halichomozi na hujulikana kama usiku wa ‘polar’ au ‘polar night’.

Hii inamaanisha katika eneo hilo hubakia kuwa kwenye giza wakati wa msimu wa baridi kali. Eneo hilo pia ni maarufu kwa milima iliyofunikwa na theluji zenye kupendeza. Mahali hapa panaweza kutembelewa katika majira ya joto au baridi.

Finland ni yenye ardhi yenye maelfu ya maziwa na visiwa, sehemu nyingi za Finland hupata kuona jua moja kwa moja kwa siku 73 tu wakati wa msimu wa joto.

Wakati huu, jua linaendelea kuangaza kwa karibu siku 73, huku wakati wa msimu wa baridi, eneo hilo halioni mwanga wa jua. Pia ni moja ya sababu kwanini watu hapa hulala kidogo tu wakati wa msimu wa jua na zaidi wakati wa baridi.

Ukiwa nchini humo unaweza kufurahia taa za kaskazini na pia kupata fursa ya kushiriki mchezo wa kuteleza kwa ubao kwenye barafu.

Uswiss, Kuanzia mwanzoni mwa mwezi Mei hadi mwishoni mwa Agosti, Uswiss huona jua likitua karibu usiku wa manane na kuchomoza karibu saa 10 alfajiri.

Hapa, kipindi cha jua kuwepo mara kwa mara kinaweza kudumu hadi miezi sita ya mwaka, kwa hivyo ukiwa eneo hilo mtu anaweza kutumia siku ndefu kwa kujishughulisha na kucheza gofu, uvuvi, kuchunguza njia za kusafiri, na mengine mengi zaidi.