GITEGA, BURUNDI

RIPOTI mpya ya shirika la usaidizi wa watoto la nchini Uingereza, Save the Children limesema majanga ya asili ambayo yamesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yamewalazimisha watu zaidi ya 100,000 nchini Burundi kuyakimbia makaazi yao katika miaka ya hivi karibuni.

Ripoti hiyo inasema mabadiliko ya tabia nchi ni jambo la kushtusha na sio tu migogoro mengine ambayo imekuwa chanzo kikubwa katika kuwafanya wengi wayakimbie makaazi yao kwa taifa hilo, lisilo na bandari lililo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambalo pia wakaazi wake wengi wapo katika maeneo ya vijijini.

Save the Children ilisema zaidi ya asilimia 84 ya watu ambao wameachwa bila ya makaazi ndani ya Burundi, imetokana na majanga asilia kuliko migogoro, na mengi yametokana na kufurika kwa Ziwa Tanganyika, ambalo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika.

Kadhia hiyo inatajwa kuwaathiri zaidi watoto ambapo Save the Children linakadiria watoto 7,200 miongoni mwa waathirika au asilimia saba ikiwa ni watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja.