LONDON, UINGEREZA

LICHA ya kuongezeka wigo wa bima au hifadhi ya jamii ulimwenguni wakati wa janga la corona, lakini zaidi ya watu bilioni nne duniani bado hawana bima hiyo.

Taarifa hizo zilitolewa wakati ilipowasilishwa ripoti mpya ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa, ILO.

Ripoti hiyo iliyotolewa inasisitiza kuwa hatua za kupambana na janga la COVID-19 hazikuwa za kutosha na zilikuwa za kutatanisha, zikipanua zaidi pengo kati ya nchi zenye kipato cha juu na kipato cha chini, na zilishindwa kutoa ulinzi wa kijamii unaohitajika ambao kila mwanadamu anastahili.

Ripoti inasema ulinzi wa jamii ni pamoja na upatikanaji wa huduma za afya na usalama wa kipato, haswa kwa wazee, na pia ikiwa kuna ukosefu wa ajira, magonjwa, ulemavu, ajali kazini, uzazi au kifo cha mlezi mkuu wa familia, na pia kwa familia zilizo na watoto.

Mkurugenzi mkuu wa ILO, Guy Ryder alisema katika ripoti hiyo kwamba nchi ziko njiapanda.Huu ni wakati muhimu wa kuchukua hatua za kupambana na janga hilo na kujenga kizazi kipya cha mifumo ya haki za ulinzi wa jamii.

Kulingana na mkuu huyo wa ILO, kwa kulinda idadi kubwa ya watu kutokana na majanga ya siku za usoni, mifumo kama hiyo ya haki za hifadhi ya jamii ni muhimu kwani huwapa wafanyakazi na wafanyabiashara usalama wanaohitaji kukabiliana nayo kwa ujasiri na kutumaini mabadiliko mengi.

Hivi sasa, ni watu milioni 475 tu ya idadi ya watu ulimwenguni ndio ambao wanalindwa na angalau faida moja ya mifumo ya hifadhi ya jamii, wakati watu bilioni 4.1  sawa na asilimia (53%) hawana uhakika wa kipato kupitia mfumo wao wa kitaifa wa hifadhi ya jamii.

Ulaya na Asia ya Kati zina viwango vya juu zaidi vya huduma za hifadhi ya jamii, na asilimia 84 ya watu wao wanapata walau faida moja ya huduma hizo.

Marekani viwango viko juu ya wastani wa viwango vya dunia, na ni asilimia 64.3%.Asia na Pasifiki ni asilimia (44%), huku mataifa ya Kiarabu yakiwa na asilimia (40%).Afrika ni asilimia (17.4%) na wana mapungufu ya wazi katika hifadhi ya jamii.