NA MARYAM HASSAN
ZANZIBAR inatarajia kuungana na mataifa mbali mbali duniani kuadhimisha siku ya utalii itakayofanyika Septemba 27 mwaka huu kisiwani Pemba.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Kikwajuni Mjini Unguja, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Leila Mohammed Mussa, alisema lengo kuu katika siku hiyo ni kukuza heshima na kuzalisha fursa kwa watu mbali mbali duniani kote.
Alisema Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) litaadhimisha siku hiyo kimataifa nchini Ivory Coast na kwa hapa Zanzibar maadhimisho hayo yatafanyika Kisiwani Pemba kwa siku mbili kuanzia Septemba 26, mwaka huu.
Alisema hatua hiyo ni moja ya mipango ya serikali ya awamu ya nane ya kuimarisha na kukuza uchumi wa kisiwa cha Pemba kwa kuvutia utalii endelevu na uwekezaji mwengine wenye manufaa.
Alieleza kuwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale itashirikiana na sekta binafsi katika kuandaa maadhimisho ya siku hiyo.
“Ili kutekeleza falsafa ya (UNWTO) Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeamua kuishirikisha sekta binafsi katika kuandaa maadhimisho ya siku hii adhimu ya utalii duniani,” alisema Lela.
Alisema mashirikiano hayo ndio yatakayoleta chachu ya kuhakikisha faida zitakazopatikana zinawafikia wananchi wote katika jamii na kuhakikisha kuwa dhana nzima ya utalii kwa wote inafikiwa.
“Sekta ya utalii ni muhimili muhimu katika uchumi wa Zanzibar hivyo ili kuhakikisha utalii unawanufaisha wengi hapa Zanzibar, ni lazima kuwe na mikakati endelevu,” alisema.
Akizungumzia kuhusu janga la Uviko 19, waziri huyo alisema kwa kiasi kikubwa limeleta athari ya kiuchumi na kijamii duniani kote, ikiwemo nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Alisema biashara ya utalii ndio ambayo imeathirika zaidi kutokana na nchi nyingi kufunga na kuweka vikwazo kwa raia wao na wananchi wengine.
Alisema kuanza tena kwa biashara ya utalii kutasaidia kufungua njia za uchumi na kupunguza athari zilizojitokeza kwa kipindi chote hicho.
Kwa kuliona hilo Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani limezingatia umuhimu wa ukuaji wa utalii jumuishi na hivyo kuifanya siku ya utalii mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya Utalii kwa maendeleo jumuishi kwa wote.
Aliongeza kuwa katika kuadhimisha siku hiyo alisema Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa utalii wameandaa shughuli za kitalii ikiwemo ngoma za asili, michezo ya ngo’mbe na ziara ya kutembelea maeneo ya kitalii.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni ya Mkamandume, Chwaka Ruins, Ras Mkumbuu, Wete Town, Chakechake na maeneo wanapopatikana Popo wa Pemba pamoja na washiriki kupanda ngalawa na kuwahimiza wananchi kujitokeza wakati wa maadhimisho hayo.