NA KHAMISUU ABDALLAH

JUMLA ya hekta 1,000 zinapotea kila mwaka kwa matumizi mbalimbali ya rasilimali za misitu ikiwemo kukata miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa na kuni.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma, aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo Ofisini kwake Maruhubi Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema imefika wakati kwa wananchi kuitumia misitu kiuendelevu na kuacha kutumia misumeno ya moto bila ya kufuata taratibu, ili miti iendelee kudumu kwa kutunza mazingira na kujikinga na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Alibainisha kuwa Idara imekuwa ikikamata watu wanaoihujumu misitu kwa kuikata kwa makusudi na kuweza kuchukuliwa hatua ikiwemo kutozwa faini.

Alisema kuanzia mwezi Januari hadi Agosti mwaka huu jumla ya watu 23 wamekamatwa kutokana na kukata miti na kuchukuliwa hatua ya kufikishwa mahakamani.

“Katika kesi hizi tunachukua hatua ya kuripoti vituo vya Polisi na baadae kupelekwa mahakamani wengi wao wanapelekwa  Manispaa ya Wilaya ya Kati na hukumu nyingi kati yao zilikuwa ni kifungo cha miezi sita jela au faini ya shilingi 1,000,000,” alibanisha.

Kaimu Said, alifahamisha kuwa zipo baadhi ya kesi pia zilizohukumiwa na Idara hiyo kwa mujibu wa sheria na kanuni kwa kuwatoza faini kulingana na kosa analopatikana nalo mtuhumiwa.

“Tukimkamata mtu ambae anatuhumiwa kukata mti mmoja basi faini yake inatakiwa isipungue shilingi 700,000 na tumekuwa tukichukua hatua hizi ili kuhakikisha wananchi wanaheshimu sheria za nchi katika kutunza mazingira yanayowazunguza,” alibainisha.

Hata hivyo, alibainisha kwamba wananchi wafahamu kuwa Zanzibar ni kisiwa kinachozungukwa na maji ya bahari hivyo kuihujumu misitu kutapelekea maafa makubwa ya kimazingira.

Hivyo, aliwasisitiza kutoka  katika matumizi ya kuni na mkaa na kwenda kwenye matumizi rasilimali ya gesi na matumizi mengine ya umeme ili kuendelea kutunza mazingira ya nchi yao.

Naye Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Hassan Juma Amour, alisema Zanzibar kwa kiasi kikubwa imehamasika katika utumiaji wa  nishati ya gesi ya kupikia majumbani.

Alisema hali hiyo, kwa kiasi kikubwa imepunguza ukataji wa miti ovyo kwa matumizi ya kuni na mkaa katika maeneo mengi ya mjini na vijijini.

Alibainisha kuwa hivi sasa soko la gesi ya kupikia hapa Zanzibar, limekuwa kwa kasi hivyo mamlaka imeona kunahitajika udhibiti na jambo hilo na linahitaji kusimamiwa kwa nguvu zote kama inavyosimamia sekta ya mafuta.

Ofisa huyo alisema, ZURA ina jukumu la kusimamia shughuli za nishati ikiwamo gesi ya kupikia majumbani, ili kuona haileti madhara kwa watumiaji.

Hivyo, aliwaomba wananchi kubadilika na kuingia katika sayansi na teknologia katika matumizi ya nishati ya gesi, ili kukinga mazingira ya nchi yao.