NA LAYLAT KHALFAN

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mwinyi Mohammed, amesema (ZATUC) itahakikisha inasimamia viwango bora vya ajira vilivyowekwa na mikataba ya kimataifa vinafikiwa na kuimarishwa zaidi.

Aliyasema hayo alipokuwa akizugumza na waandishi wa habari Jambiani Wilaya ya Kusini mkoa wa kusini Uguja kuhusiana na haki na wajibu kwa mfanyakazi.

Alisema kuna wimbi kubwa la wafanyakazi wanaendelea kufanyakazi zisizokuwa na staha, heshima huku wakiendelea kudharaulika kwa waajiri wao siku hadi siku kinyume cha utaratibu.

Alisema miongoni mwa uimarishaji hayo ni kutoa fursa katika ajira ikiwemo mafunzo, kupandishwa vyeo sambamba na motisha katika kazi, ili wafanyakazi wafanye kazi zao wakiwa sehemu salama.

“Hichi chama kinajukumu kubwa la kusimamia wafanyakazi na kulinda maslahi yao, haki zao na wajibu katika kufanyakazi ili kuondokana na manyanyaso ya muda mrefu”, alisema Katibu huyo.

Alifahamisha kuwa, moja ya kazi kuu ya chama ni kuhakikisha suala la kudai na kutetea haki kwa wafanyakazi wote wanalielewa, ili inapostahiki wapatiwe haki zao za msingi za kazi zao wanazozifanya.

Sambamba na hayo Katibu Mkuu (ZATUC), alisema ili kuimarisha huduma bora kwa mfanyakazi ni kuhakikisha wanashirikiana na wadau wengine kutatua migogoro katika sehemu za kazi kwa misingi ya kisheria, ili kuleta tija na haki ziweze kupatikana.

“Kwa upande wa muajiri siku zote yeye kazi yake ni kuhimiza wajibu wa mfanyakazi, lakini mambo mengine anaona hayamuhusu kwa kuwa anahisi wafanyakazi watajua sheria zao za kazi na kupata haki zao”, alisema.