Kujenga jengo la gorofa 5

NA HAFSA GOLO

SERIKALI ya Zanzibar, imeanza kutekeleza mradi wa kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama ndani ya Wilaya tatu  za Unguja, sambamba na ujenzi wa ofisi ya ghorofa tano ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) utakaotumia dola milioni 92.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano ZAWA, Amina Abdalla Daud, wakati akizungumza na Zanzibarleo  ofisini kwake Mabluu alitaja  Wilaya zitasogusa mradi huo  ni Magharibi ‘A’, Magharibi ‘B’ na Wilaya ya Kati,

Alisema mradi huo  utachimba visima 63, vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 792,000  kwa saa  ambao utahusisha zoni tatu ikiwemo Mfenesini, Dole, Dimani,  Mkorogo  na Kitundu.

Aidha, alisema zoezi hilo litakuwa pamoja na uwekaji wa matangi 15, yenye uwezo wa kuhifadhia maji lita milioni 152.45 na kusambaza mabomba kilomita 461.

“Tayari hatua za utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri katika  maeneo mbali mbali ikiwemo uchimbaji wa visima ,uwekaji wa matangi na usambazaji wa mabomba na hakuna changamoto iliyojitokeza hadi sasa”,alisema.

Alibainisha kwamba mradi huo utazinufaisha shehia 36 na kuwanufaisha wananchi wapatao 286,798 ndani ya Wilaya tatu zilizopita mradi huo. Amina, alisema ZAWA itahakikisha inasimamia kwa karibu, ili kuona miundombinu inayojengwa inakidhi viwango kwa lengo la kutimiza azma ya serikali ya kumaliza changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.

“Utakapokamilika mradi huo kilio cha ukosefu wa huduma ya maji na salama kwa wananchi kitamalizika”,alisema.