NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali, amesema kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni hatua muhimu katika usimamizi wa taasisi za uwekezaji na mali za umma nchini.

Jamal aliyasema hayo wakati akiwasilisha mswaada wa sheria ya kuanzisha ofisi ya msajili wa hazina na usimamizi wa mali za umma katika baraza la wawakilishi linaloendelea visiwani Zanzibar.

Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Mashirika ya Umma kwa lengo la kuendesha biashara na kutoa huduma katika jamii ili kuimarisha uchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Hivyo alisema katika kuyasimamia Mashirika hayo, Serikali iliona haja ya kuanzisha sheria itakayosimamia mashirika hayo na kufanya hivyo kutaongeza tija kwa wananchi na ufanisi wa mashirika hayo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Hata hivyo alisema kwamba kutokana na mabadiliko ya maendeleo ya kiuchumi, Serikali iliamua kuwekeza kwa njia tofauti zikiwemo kununua hisa, kuingia mashirikiano ya kibiashara, sekta binafsi pamoja na kuwekeza katika mitaji.

Alifahamisha kwamba hali hiyo ilipelekea kuundwa kwa sheria mpya ya mitaji ya Umma nambari 4 ya mwaka 2002, ambayo iliimarisha usimamizi wa Mashirika ya Umma na Kampuni za Serikali katika kuimarisha uchumi ambayo yaliongeza mapato ya Serikali kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali, ulipaji wa gawio pamoja na kutoa ajira.

Hata hivyo alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kupitia sheria hiyo lakini serikali imeonekana ipo haja ya kupitiwa upya sheria hiyo kwa lengo la kuimarisha usimamizi zaidi wa Mali pamoja na Mashirika ya mma.

Hivyo alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa Sheria ya Kuanzisha Ofisi ya Msajili wa Hazina na Usimamizi wa Mali za Umma na kufuta Sheria ya Mitaji ya Umma nambari 4 ya mwaka 2002 ni kuimarisha usimamizi wa Mashirika ya Umma ili yaweze kufanya kazi kwa ufanisi, kutoa huduma bora na hatimae kupelekea kuongezeka mapato ya Serikali kupitia gawio na kodi zitakazolipwa na mashirika hayo.