NA MADINA ISSA
WAZIRI wa utalii na mambo ya kale, Lela Mohammed Mussa amezindua safari za ndege ya kampuni ya Africa Stay kupitia ndege ya Global Air ways itakayofanya safari zake za moja kwa moja kati ya Afrika Kusini na Zanzibar
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya ndege hiyo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), Lela, alisema hatua hiyo inakusudia kukuza sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.
Alisema huo ni mwanzo mzuri katika kuona sekta ya utalii ambayo ni chanzo kikuu cha uchumi wa Zanzibar inakuwa baada ya kipindi cha mripuko wa janga la Covid -19 lililoathiri kwa kiasi kikubwa sekta hiyo
Hivyo, aliwaomba wananchi kuonesha utayari wao katika kuimarisha utalii kwa kuzingatia tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kuvaa barkoa,kuepuka mikusanyiko isiyokuwa na lazima pamoka na kuchanja ili kuwatoa hofu wageni dhidi ya usalama wa afya zao
Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk. Mohammed Juma Abdallah, alisema lengo la serikali ni kuona wanapokea idadi kubwa ya wageni wakiwemo watalii wenye hadhi ya juu ili kukuza uchumi wa nchi
Mapema Mkurugenzi wa kampuni ya Africa Stay, Marian Sandu, alisema wamefurahia mazingira ya Zanzibar na kuahidi kuhamasisha wageni wengine zaidi kuitembelea Zanzibar.
“Mandhari mazuri yaliyopo Zanzibar yataendelea kuwahamaisha wageni wa mataifa mengine ili kuona watu wao wanafika Zanzibar,” alisema.
Ndege hiyo imepokelewa ikiwa na watalii 170 kwa kuanzia itakuwa inawasili wiki mara moja na baadae itafanya safari zake mara tatu kwa wiki ambapo katika mapokezi hayo viongozi mbali mbali wa serikali na taasisi binafsi akiwemo waziri wa Ujenzi Mawasikiano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali walihudhuria.