NA MWANDISHI WETU

TAASISI ya Viwango Zanzibar (ZBS) inashikilia na kuiondoa sokoni mafuta ya kulaibnishia mitambo aina ya DG OIL baada ya kubainika kuwa ipo chini ya kiwango.

Akizungumza katika ghala lililohifadhiwa bidhaa hiyo Mwera Mtofaani, Mkurugenzi Usimamizi Ubora wa bidhaa kutoka ZBS, Msimu Juma Ramadhan, alieleza kuwa pamoja na kukosa ubora, mfanyabiashara aliyeingiza bidhaa hiyo, alikiuka taratibu za ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje.

Alieleza kuwa mfanyabiashara huyo Darajani General Traders, aliingiza bidhaa hizo sokoni kabla ya kutolewa kwa majibu ya ukaguzi jambo ambalo ni kinyume na sheria ya ZBS.

“Ili kuondoa msongamano bandarini, mfanyabiashara anaweza kuruhusiwa kuondoa mizigo bandarini na kutakiwa kuihifadhi hadi majibu ya ukaguzi yanapotoka na kama viwango vimefikiwa unaruhusiwa lakini ukiwa haujakidhi viwango hatua huchukuliwa,” alieleza Msimu.

Alieleza kuwa mfanyabiashara huyo baada ya kupewa ruhusa ya kuondoa mzigo wake bandarini, alipaswa kusubiria majuibu ya ukaguzi jambo ambalo hakulifanya badala yake aliingiza mzigo sokoni.

Hivyo mkurugenzi huyo, aliwataka watumiaji wa bidhaa hiyo kutoinunua badala yake watoe taarifa katika taasisi hiyo huku wakiendelea na taratibu za kisheria.

“Tumeanza kukusanya mzigo huu kutoka katika maghala yaliyopo hapa na maeneo mengine ambapo tutaushikilia hadi pale mfanyabiashara aliyeuingiza atakapourudisha ulipotoka au kuuangamiza,” alieleza Msimu.

Akitaja kiwango kuhusiana na mzigo huo, Mkurugenzi huyo alisema ni mageloni na katuni 2,212 ya ujazo wa lita 20 na lita tano na kueleza kuwa pamoja na kuuzuia mzigo huo, mfanyabiashara huyo atatozwa faini pamoja na kutakiwa kugharamia gharama za uangamizaji iwapo atashindwa kuurudisha nchi ulipotoka.

Akizungumzia matokeo ya ukaguzi wa bidhaa hiyo, Kaimu Mkuu wa Ukaguzi na Usimaizi Ubora, Said Haroub Said, alieleza Mwakilishi wa mfanyabiashara huyo aliruhusiwa kutoa mzigo huo na alikubali kutoa mzigo huo na kuuzuia hadi yatakapotolewa majibu ya maabara.