NA LAYLAT KHALFAN
SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO), limefanikiwa kusambaza huduma ya umeme katika kijiji cha Bumbwini Kiongwe kwa asilimia 100 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Kampeni zake.
Meneja Mkuu wa Shirika hilo, Mshenga Haidar Mshenga, aliyasema hayo katika mkutano wa Walimu Wakuu na watendaji wa kituo cha afya Bumbwini Kiongwe mkutano uliofanyika kituoni hapo, wilaya ya Kaskazini ‘B’, Unguja.
Alisema tayari shirika hilo limeshaweka transfoma na wananchi wanaweza kujiunga na huduma hiyo ili kuweza kujiletea maendeleo kupitia nishati hiyo.
Aidha, Meneja huyo alifahamisha kuwa, kupatikana kwa huduma hiyo kwa kijiji hicho kutawarahisishia wananchi kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo ya haraka na kufikia malengo waliyojiwekea.
Alisema katika kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho, Shirika hilo linakusudia kuunga umeme katika kituo cha Afya na skuli bila ya malipo yoyote kutokana na kuwepo kwa umuhimu wake kwa sekta hizo.
“Kwa vile watoto wetu wanasoma katika skuli hizi na kupata matibabu ndani ya kituo hiki, tutawaungia umeme bure ili kuwaondolea usumbufu pale patakapohitajika kutumia vifaa vya umeme kwenye majukumu yenu”, alisema.
Naye Mkuu wa Kituo cha Afya kijijini hapo, Dk. Said Omar Mtawa, alilipongeza shirika hilo kwa kujitolea kuwapatia huduma hiyo muhimu bure kwani awali walikuwa wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kutokana na kukosa huduma hiyo.
Mapema Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Khamis Mrisho Khamis, alisema amepata faraja kwani hatua hiyo itawarahisishia kuchapisha mitihani yao kwa urahisi badala ya kugharamika kwenda masafa marefu kwa ajili ya kutafuta huduma hiyo.
Nao wanafunzi wa skuli hiyo, walilishukuru shirika hilo kwa uamuzi wake waliochukua wa kuwapatia huduma ya umeme skulini hapo kwani itawasaidia kujifunza kwa vitendo baadhi ya masomo ya sayansi na kupelekea kufanya vyema mitihani yao.
Walisema wamezoea kusoma kwa nadharia wakati mwengine wanashindwa kujibu suala lilivyo kutokana na kushindwa kujifunza kwa vitendo baadhi ya mambo na kusababisha kushuka kwa ufaulu ndani ya skuli yao.
Zaidi ya shilingi millioni 200, zimetumika kwa ajili ya kuwasambazia wananchi huduma ya umeme ndani ya Kijiji cha Bumbwini Kiongwe ikiwa ni ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi.