NA ASIA MWALIM

WAKALA wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeitaka jamii kuwa na mwamko wa kutoa taarifa sehemu husika endapo watabaini kuchinjwa wanyama sehemu zisizorasmi ikiwemo kwenye makaazi ya watu.

Mkuu wa Ukaguzi wa Chakula, Suleiman Akida, aliyasema hayo alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Mombasa Zanzibar.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuepuka suala la kuchinjwa wanyama kiholela katika maeneo yasiyo salama, jambo ambalo huhatarisha usalama kwa watumiaji baada ya kushindwa kufanyiwa vipimo.

Aidha, alisema kufanya hivyo kutasaidia kupata bidhaa za chakula chenye kiwango kinachohitajika kwa kulinda afya ya mlaji na kuzingatia usalama wa matumizi ya binaadamu.

Alisema ubora na usalama wa chakula hauonekani kupitia macho wala ukubwa wa mnyama hivyo ni vyema kufuata utaratibu wa kuchinja sehemu zilizoruhusiwa, ili kufanyiwa vipimo kabla ya matumizi ya chakula.

Alifahamisha kuwa kuna umuhimu wa kupimwa ubora unaohitajika kwa wanyama ili kuzuia vitu vilivyo haribika na visivyofaa kwa matumizi ya chakula kwa binaadamu.

“Watu wengi wamezoea kuchinja wanyama kienyeji, hawajui umuhimu wa kufanyiwa ukaguzi wala hawajali afya za wengine wanachojali ni kuchinja na kupata nyama ya kula” alisema.

Alisema juhudi zinahitajika kwa wananchi kushirikiana na serikali za mitaa, ili kutokomeza kadhia hiyo sambamba na kuzuia suala la wizi wa maifugo.

“Tunaamini kuwa jamii itashiriki kikamilifu kutoa mashirikiano kwa viongozi wa shehia watu wote watafuata sheria na tutapunguza tabia ya wizi wa mifugo” alisema.