Wananchi watoa ya moyoni
NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WANANCHI kisiwani Pemba wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza ahadi yake ya kurudi kwa wananchi kisiwani humo kusikiliza kero zinazowakabili.
Itakumbukwa kuwa mnamo Agosti 31 mwaka huu, Dk. Mwinyi alifanya ziara ya siku nne kisiwani humo ambapo alitembelea miradi mbalimbali iliyomo katika mikoa miwili na wilaya nne kisiwani humo.
Katika ziara hiyo ya Dk. Mwinyi mbali ya kutembelea miradi ya maendeleo, pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kisiwani Pemba kwa kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu wa mwaka jana, sambamba na kusikiliza kero zao zinazowakabili.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti baada ya kumalizika kwa ziara hiyo, wananchi hao walisema wamefarajika sana kwa hatua za kiongozi huyo kutimiza ahadi ya kurudi tena kwao baada ya kushinda nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Khatibu Mshindo Faki alisema kuwa akiwa katika kampeni za kuwania nafasi ya urais, Dk. Mwinyi aliahidi kurudi tena kwa wananchi kusikiliza kero zao zinazowakabili.
“Tumefarajika sana ameonesha kwamba yeye ni kiongozi muungwana na anayejali wananchi wake, amerudi kwetu kuja kutusikiliza changamoto zinazotukabili”, alisema Khatib Mshindo Faki mkaazi wa Kiuyu Mbuyuni.
Faki alisema kuwa anaamini hatua hiyo aliyoichukua Dk. Mwinyi ya kukutana na wananchi na kuzisikiliza kero za wananchi itamsaidia kujua ukubwa wa matatizo waliyonayo na sio kudanganywa na baadhi ya watendaji wake.
Naye Rajab Ali Mkanda mkaazi wa Micheweni, alisema Dk. Mwinyi amefanya jambo zuri kushuka chini kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi, kwani kama angesubiri ofisini angeishia kudanganywa.
“Hapa kuna huduma mbali mbali ambazo tunazikosa ikiwemo maji, barabara, dawa hospitali hamna, hivyo ikiwa hakushuka kwa wananchi kuwasikiliza asingeliyajua na tungeendelea kuzikosa huduma hizo”, alisema Mkanda.