NA KHAMISUU ABDALLAH

ZAIDI ya vyombo 10 vya uvuvi na abiria vimekamatwa kwa makosa ya kutokuwa na leseni na mkosa mengine huko Mkokotoni na Fungu refu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Hayo yamebainika wakati Mkuu wa kitengo cha Majahazi kutoka ZMA, Anas Omar Anas na ujumbe wake wa watu sita walipofika katika bandari hizo kwa lengo la kufanya ukaguzi wa vyombo na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kukata leseni za vyombo vyao.

Aidha alisema sasa wakati umefika kwa wamiliki kukata leseni hizo, kwani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa punguzo la ada ya leseni kutoka shilingi 60,000 hadi 10,000 kwa lengo la kuona kila chombo kinakatiwa leseni.

Alisema ni jukumu la manahodha na mabaharia kuhakikisha vyombo vyao vinaleseni kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na serikali.

Anas alitoa muda wa wiki mbili kwa wamiliki hao kuhakikisha wanakata leseni kwa faida yao na yoyote atakaebainika anakiuka sheria hiyo basi chombo chake kitazuiliwa kufanya kazi.

“Nawapa wiki mbili mhakikishe mnakata leseni za vyombo vyenu na mkidharau kinachofuata ni kuvizuia visifanye kazi vyombo vyote vitakavyokuwa havina leseni hata kwa nahodha na baharia ambae atakuwa hajakamilisha taratibu za usafiri wa baharini,” alisisitiza.