NA HANIFA SALIM, ZUHURA JUMA, PEMBA
WAKULIMA wa kilimo cha Mchaichai kisiwani Pemba wamelalamika shirika la Biashara la ZSTC kuwashushia bei ya mafuta ya mchaichai, licha ya kuwa soko la bidhaa hiyo liko pale pale.
Wakizungumza na waandishi wa habari wakulima hao walisema, kinachowashangaza ni kwamba soko la mafuta ya mchaichai halijashuka, ingawa wakulima wameshushiwa bei kutoka 200,000 hadi kufikia 120,000 jambo ambalo limewatia hasara kubwa.
Walieleza kuwa, katika soko la kimataifa lita moja ya mafuta ya mchaichai wananunua shilingi 320,000 ingawa shirika linanunua kwao kwa shilingi 120,000 jambo ambalo linawatia unyonge, kwani wao ndio wanaofanya kazi kubwa.
“Mwanzo shirika lilikuwa linanunua kwetu lita moja kwa shilingi laki mbili na wao wanapata faida ya 120,000, lakini kinachotushangaza wamekuja kutushushia bei na wala soko halijashusha bei, hivyo tumepata hasara kubwa na tunadaiwa”, walifafanua.
Mmoja wa wakulima hao Khamis Ramadhan Faraji mwenye shamba lake Mbiji Mkoani alisema, walihamasishwa kulima mchachai, ingawa kwa sasa wameanza kuwavunja moyo kutokana na bei waliyowekewa.
“Sisi ndio tunaofanya kazi kubwa, tunawalipa watu watusaidie lakini kinachotushangaza na kutusikitisha ni kuona shirika wanachukua wao pesa kubwa kuliko sisi wakulima, hii sio haki kutokana na kuwa soko la bidhaa hiyo halijashuka”, alisema mzee huyo.
Alisema, shamba lake lina ukumbwa wa ekari tatu na nusu ambalo huzalisha mafuta mengi baada ya mavuno, ila kinachowasikitisha ni wameanza kuvuliwa matumaini waliyokuwa nayo kutokana na zao hilo.
“Watu ambao niliwaajiri kunisaidia katika shamba langu walinishitaki na kunipeleka mahakamani kwa sababu niliwapa kiwango ambacho hakikufika makubaliano, niliwambia kwamba bei imeshuka lakini hawakunielewa, kwa kweli nilidhalilika mtu mzima”, alielezea.
Aidha alisema, kwa sasa kiwanda ambacho kilikuwa kinawasaidia kukamulia mafuta hayo kimeharibika, jambo ambalo linawarejesha nyuma zaidi kiutendaji, hivyo aliiomba Serikali kuwatengenezea ili kuondokana na changamoto hiyo.
Salma Said Rashid mkulima wa shamba la mchaichai Chonga Wilaya ya Chake Chake alisema, wamekuwa wakipata hasara kutokana na kushuka kwa bei na kukosekana kwa kiwanda cha kukamulia mafuta hayo.
“Tunapata shida wakati tunapotaka kupeleka mchaichai wetu kiwandani, kwa sababu tukipeleka kiwanda cha Mgelema muhusika mkuu anatwambia kiwanda chake ni cha kukamulia majani ya mkarafuu na sio mchaichai na kule Mtakata mafuta hayatoki kwani nyungu zao ni mbovu,” alisema.
Alisema kuwa, walikuwa wanapata faida wao na wananchi wengine, kwani wakinunua mchaimcha katika maeneo tofauti ili kuwasaidia kukuza kipato chao, ingawa kwa sasa wanashindwa.
“Kwa kweli wananchi wengi ilikuwa wanafaidia za bidhaa hii, kwa sababu licha ya kulima sisi pia ilikuwa tunanunua kutoka kwa wakulima wadogo wadogo angalau na wao wakipata kujikwamu kimaisha, lakini kutokana na bei ilivyo sasa tumeshindwa kununua”, alisema Salma.