BLOEMFONTEIN, AFRIKA KUSINI

RAIS wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela baada ya kukaidi agizo la mahakama kuhusu kesi ya rushwa dhidi yake, ameruhusiwa kumaliza kifungo chake akiwa nyumbani kufuatia hali yake ya afya.

Maofisa wa gereza walitangaza msamaha huo wa kiafya miezi miwili tangu Zuma aanze kutumikia kifungo hicho.

Zuma mwenye umri wa miaka 79 amekuwa akilazwa katika hospitali moja nje ya mahakama hiyo tangu Agosti 6.

Mnamo Agosti 14 alifanyiwa upasuaji ambao maelezo yake kamili hayajaelezwa yanahusu nini.Idara ya Magereza ilisema uamuzi wao ulitokana na ripoti ya kiafya waliyopata kuhusu Zuma.

Hata hivyo walisema atahitajika kufuata masharti atakayopewa na watamfuatilia kuhakikisha anamaliza kifungo chake.