NA KHAMISUU ABDALLAH

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imeandaa muongozo utakaotumika kwa wauzaji wa rejareja wa nishati ya gesi Zanzibar ili kuondoa changamoto ya kiusalama.

Hayo yalielezwa na Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Hassan Juma Amour, wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Maisara mjini Unguja na kueleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kubaini changamoto ya uuzaji usiofuata misingi ya usalama.

“Muongozo huo umeandaliwa mwezi Julai, mwaka huu na umeshakamilika na hivi sasa upo katika hatua ya kwanza ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuufahamu muongozo huo,” alieleza Hassan.

Alibainisha kwamba tayari elimu hiyo imeanza kutolewa kwa waingizaji wakubwa, wasambazaji na wauzaji rejareja wa nishati hiyo hapa Zanzibar.

Alisema lengo la muongozo huo ni kuhakikisha wana kanuni ambazo zitawaongoza wauzaji wa nishati hiyo wa rejareja kwani awali walikuwa wakiuza nishati hiyo bila ya kuwa na leseni.

Aidha Hassan alibainisha kuwa lengo jengine la muongozo huo ni kupunguza idadi ya wafanyabiashara wanaouza nishati hiyo kwa rejareja ili kupata ubora katika sekta hiyo muhimu.

Akizungumzia changamoto ya uchanganyaji wa bidhaa za kawaida na nishati hiyo, alisema ilijitokeza katika uombaji wa leseni kutokana na wadau wa sekta ya gesi kutokaa pamoja na kuliangalia jambo hilo.

“ZURA, ZIPA, Manispaa, KMKM na wadau wengine, tulikuwa hatujakaa chini kuangalia chanzo cha hili tatizo lakini baada ya kukaa pamoja tumebaini changamoto ipo katika upande wa leseni mwananchi anakwenda kuomba leseni na anapewa leseni ya kuuza bidhaa zake za chakula au vifaa vilivyotumika kupitia leseni ile ile anaingiza mitungi ya gesi na kuuza,” alisema.