NA KHAMISUU ABDALLAH

MASHINDANO yajulikanayo ‘ZURA Nakupenda Marathon 2021’ yenye kauli mbiu yake mbio ya upendo inatarajiwa kufanyika Oktoba 16 mwaka huu katika viwanja vya Mnazimmoja.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo katika ukumbi wa ZURA Maisara, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Khamis Juma, amewaomba walioandaa mashindano hayo, kuona mbio hizo zinafanyika kila mwaka ili kusaidia watoto wa kike waliokuwepo maskulini kupata taulo za kike.

Alisema wazo la kumfikiria mtoto wa kike ni jambo muhimu sana na lakupongezwa kwani wapo wasichana wengi wanahitaji huduma hiyo.

Aliwapongeza waliowaza wazo hilo ikiwemo Creative Consultancy Zanzibar Limited na Mamlaka ya Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) kudhamini mashindano hayo, lenye lengo la kumfikiria mtoto wa kike katika maeneo mengi ya Zanzibar ambao wanakosa huduma hiyo.

Mbali na hayo alishauri kuwa sio tu katika marathon ndio wasaidie watoto wa kike, lakini yapo maeneo mengi ambayo watoto wa kike wanahitaji kusaidiwa.

Katibu Ali, alibainisha kuwa wizara ipo tayari kusaidia mbio hizo kwa kutoa wanafunzi na kuwasimamia, ili kuhakikisha wanafanikisha shughuli hiyo muhimu.

Mwakilishi kutoka ZURA Nakupenda Marathon 2021, Benedict Anthony alisema mbio hizo zitafanyika katika viwanja vya Mnazimmoja na kumalizika katika viwanja hivyo, zitakazoshirikisha mbio za kilomita 1 ambayo itawashirikisha watoto au wanafunzi kutoka skuli mbalimbali wakiwemo walemavu, kilomita 5, kilomita 10  na kilomita 21.

Alisema shughuli rasmi zitaanza Oktoba 14 kwa kufanya usafi katika njia zote zitakazotumika katika marathon hiyo, kwa kushirikiana na wasafisha Zanzibar na Oktoba 16 kuadhimisha siku ya unawaji mikono.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mtu anaetaka kushiriki mashindano hayo kiingilio kitakuwa shilingi 25,000 kwa mtu mmoja, ambayo itasaidia katika shughuli mbalimbali ikiwemo medali za washiriki wa mbio hizo na mchango katika kununua taula za kike.

Sambamba na hayo alisema siku hiyo pia kutakuwa na burudani mbalimbali zitakazoshirikisha wasanii kutoka Zanzibar wakiwemo Densa na mabanda ya tasisi mbalimbali za serikali ikiwemo ZURA kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi.

Akizungumzia lengo la kuanzisha mbio hizo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kununua taula za kike, kwa wasichana ambao wapo skuli kwa ajili ya kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

Hivyo, aliwaomba wananchi wa Zanzibar hasa vijana kujitoleza katika mbio hizo ambazo zitasaidia kifikia ndoto za wanawake wa Zanzibar hasa wasichana.

Rais wa Chama cha Riaza Zanzibar, Dk. Abdul- hakim Cosmas Chasama, alisema kuwepo kwa ZURA   nakupenda marathon ni muendelezo wa mikakati ya chama chao, kuhakikisha mchezo huo unaendelea kufanyika Zanzibar na kufufua mbio nyengine ambazo zilikuwa zikifanyika huko nyuma.