NA KHAMISUU ABDALLAH

FAMILIA ya Zainab Mohammed Amour, baada ya kumalizana na mshitakiwa ,Abeid Rahim Othman, hatimae mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe imeiondosha kesi hiyo.

Hakimu Mwanaidi Abdalla Othaman, alitoa uamuzi huo baada ya upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Salum Ali, kuiomba mahakama kuiondoa kesi hiyo, kwani mashahidi hawapatikani baada ya mshitakiwa na mlalamikaji wameshamalizana kifamilia.

Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 35 mkaazi wa Dole, alikuwa akikabiliwa na tuhuma za wizi kinyume na kifungu cha 251 (1) (2) (a) cha sheria ya adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa huko Dole mshitakiwa huyo aliiba matofali 500 yenye thamani ya shilingi 600,000 kwa kukisia mali ya Zainab Mohammed Amor kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo, alidaiwa kulitenda Novemba 22 na 23 mwaka jana usiku saa zisizofahamika.