WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani Joe Biden ametia saini mswada wa kuepusha kufungwa kwa shughuli za serikali na kuipatia serikali fedha hadi mwezi wa Desemba.
Fedha hizo zitatumika pia kwa ajili ya misaada kwa waliokumbwa na maafa ya kimbunga na pia kwa ajili ya wakimbizi kutoka Afghanistan.
Hata hivyo kupitishwa hati hiyo kumeepusha mgogoro mmoja pekee wakati vyama vya siasa vinajinoa kwa mvutano juu ya namna ya kuiongezea serikali kiwango cha kukopa kabla Marekani kuwemo katika hatari ya kushindwa kulipa madeni yake.
Sheria hiyo ilihitajika ili kuiwezesha serikali kuendelea na shughuli zake baada ya mwaka wa bajeti kumalizika.
Wabunge 254 waliunga mkono hati hiyo wakati 175 walipinga.
Kwenye baraza la seneti hati hiyo iliungwa mkono na maseneta 65 na ilipingwa na maseneta 35.
Baada ya kuutia saini mswada huo rais Biden alisema bado pana kazi kubwa inayohitaji kufanyika.