NA RAYA HAMAD, OMKR   

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak ameitaka Tume ya UKIMWI Zanzibar kubuni mikakati itakayosaidia kuibua mbinu mpya za kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI.

Dk. Shajak alieleza hayo alipofanya mazungumzo na viongozi na watendaji wa Tume ya UKIMWI ambapo alisisitiza kuwa jitihada zinazofanyika hivi sasa katika kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI yaende mbali zaidi kwani dunia hivi sasa nguvu kubwa imewekezwa kwenye kupambana na virusi vya corona.

Alisema ugonjwa wa corona umeipelekea jamii kujisahau kama ugonjwa wa UKIMWI bado upo, hivyo Tume iendelee kuchukua nafasi yake katika kuelimisha jamii na kuhakikisha hakuna maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI ifikapo mwaka 2025.

“Juhudi zetu zilenge mafanikio na kufikiria njia mbadala za kutatua matatizo yaliyopo, mpango mkakati wa nne ni vyema sasa ukaangalia mawazo mapya yatakayotuvusha hapa tulipo ili tuondokane na maradhi ya UKIMWI”, alisisitiza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Tume ya UKIMWI, Dk. Ahmeid Khatib alimuelezea katibu mkuu kuwa katika kufikia malengo ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tume ina wajibu wa kutayarisha mkakati maalum na wadau wote wana jukumu la kuufuata mkakati huo.

Tume ya UKIMWI inaendelea na matayarisho ya mkakati wa nne wa UKIMWI utaogusa sekta zote kama taasisi za serikali ama binafsi pamoja na jamii kwa vile wadau wote ni wa mapambano ya UKIMWI na hivyo ni wajibu wa kila anaeguswa kuhakikisha malengo ya nchi na dunia yanafikiwa.

Alisema mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti maradhi ya UKIMWI yamepelekea Zanzibar kufikia chini ya asilimia moja ya kiwango cha maambukizi ambapo nchi chache zimeweza kufikia malengo haya na kuifanya Zanzibar iwe ni moja kati ya nchi zenye mafaniko

Dk. Ahmeid alisema hadi kufikia mwaka 2020 malengo na shabaha za dunia ni kuhakikisha kuna 90 tatu ambazo zinafikiwa, na Zanzibar imefanikiwa kufikia asilimia 90 na alihakikisha asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanaojitambua ni asilimia 94, wanaojitambua na wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI ni asilimia 98 na wanaotumia dawa ambao wameweza kuvishusha virusi ndani ya mwili ni asilimia 93.