NA ASHURA MWINYI, WUBU

AKIWA kwenye kampeni za kuwania urais wa Zanzibar na hata alipofanikiwa kuupata Dk. Hussein Ali Mwinyi, sera yake kuu ni uchumi wa buluu.

Uchumi wa buluu unatokana na matumizi ya rasilimali za bahari katika kukuza uchumi, ambapo inaaminika kuwa bahari ya Zanzibar ina rasilimali zinazoweza kuviondoa visiwa hivi katika hali ya uchumi uliopo hivi sasa na kuwa kwenye hali nzuri.

Hata hivyo fursa za uchumi wa buluu zilizopo Zanzibar kwa miaka mingi hazijatumiwa ipasavyo, ndio maana lengo la Dk. Mwinyi kuingia na sera hiyo, ni kutaka kuhakikisha malighafi zilizopo baharini zinatumiwa kikamilifu.

Uchumi wa buluu unahusisha mambo mengi yakiwemo utalii, uvuvi, rasilimali za mafuta na gesi, bandari, usafiri na hata usafirishaji kwa njia ya maji.

Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi, inaamini kuwa endapo sekta hizo zitawekezwa vizuri na wananchi kuwezeshwa hakuna sababu ya nchi isipige hatua za maendeleo.

Mbali na serikali ya Mapinduzi kuuona uchumi wa buluu kama fursa nzuri, hata serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), imeamua kuiunga mkono kwa vitendo azma ya Dk. Mwinyi kuimarisha uchumi wa buluu.

Kwa bahati njema, miongoni mwa malengo ya kuanzishwa mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha 2009/2010 chini ya sheria ya mwaka 1998 iliyorekebishwa 2007, ni kuhakikisha uchumi wa buluu unaimarika na kuwanufaisha Watanzania.

Ili kufikia lengo hilo, mnamo mwaka 2020, sheria zote zilifutwa na kuanzishwa mpya ya kusimamia na kuendeleza uvuvi wa bahari kuu ya mwaka 2020 pamoja na kanuni zake (2021).

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk. Emmanuel Andrew Sweke, alisema kuimarisha na kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, kunakwenda sambamba na uwekaji mazingira bora.

Alisema mazingira hayo ni pamoja na kutoa vivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika mpango huo.

Aidha, alieleza kuwa mamlaka hiyo ni chombo cha ulinzi kwa wahalifu kutoka nje ya nchi wanaopora rasilimali zilizopo katika bahari Hindi inayoizunguka nchi ya Tanzania, ili kuhakikisha hakuna uingiaji holela wa meli za kigeni.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za Mkurugenzi huyo Fumba wilaya ya Magharibi ‘B’, Dk. Sweke alisema lengo la kuasisiwa mamlaka ni kusimamia, kuratibu na kuendeleza shughuli za uvuvi katika ukanda wa uchumi wa bahari (Economic Zone) wa Tanzania.

Ukanda huo una ukubwa wa kilomita mraba 223,000, takriban asilimia 24 ya eneo lote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema nyenzo kuu inayoongoza mamlaka hiyo ni sheria na kanuni pamoja na ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kipo madarakani kwa sasa.

Alifahamisha kuwa, utekelezaji huo unatokana na maelekezo na maagizo ya viongozi wakuu wa nchi na dira mbalimbali za kitaifa kutoka serikali zote mbili zinazounda muungano wa Tanzania katika kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu unaleta tija kwa wazawa na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.

Aidha alieleza kuwa, mamlaka ina jukumu la kuandaa, kutekeleza na kutathimini sera ya uvuvi wa bahari kuu pamoja na kutoa leseni kwa meli za uvuvi zinazovua katika ukanda wa uchumi wa bahari.

Jukumu jengine la mamlaka, ni kufanya tafiti za uvuvi katika ukanda wa bahari kuu na mambo mengine yanayohusiana na sekta hiyo, ingawa kisheria hairuhusiwi kujishughulisha na uvuvi.

Akifafanua zaidi, alisema kuwepo kwa kanuni ni jambo muhimu kwa vile inakwenda sambamba na sheria ambazo zitaongoza kwa ufanisi na kuimarisha ulinzi wa ukanda wa bahari kuu pamoja na kuweka masharti nafuu hasa kwa wazawa, na tayari rasimu yake imesainiwa na mawaziri husika.

Alisema kwamba kanuni zimelenga unafuu katika upatikanaji leseni kwa wazawa kwa vipindi vya kila baada ya miezi mitatu, sita na miezi 12, hata hivyo, kwa wageni ni tofauti kwani wanapaswa kukata leseni mara moja kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo alisema katika mikakati yake, mamlaka imeweka mazingira wezeshi kwa wazawa kwa kupunguza gharama za uvuvi zinazohusika na usimamizi ikiwemo leseni ikizingatiwa kuwa uvuvi wa bahari kuu una gharama kbwa.

Aliitaja fursa nyengine kwa wazawa ni kutohitajika wakala wakati wa kuomba leseni, ikilinganishwa na wageni na unafuu katika malipo ya leseni kwa uvuvi unaotumia ndoana.

Akifafanua, Dk. Sweke alisema wazawa wanalipia dola 8,000 kwa mwaka, tofauti na wageni ambao wanapaswa kulipia dola 50,000 za Kimarekani.

Kwa uvuvi wa kuzungusha (purse seine), alisema malipo kwa wageni ni 70,000 wakati wazawa ni dola 21,000 ikiwa punguzo la asilimia 70.

Aidha, alisema sheria na kanuni mpya zimeruhusu wawekezaji wa ndani kuingia ubia na makampuni kutoka nje ya nchi.

Kama hiyo haotoshi, alisema mamlaka imeweka mazingira wezeshi kwa wazawa ili waongeze uzalishaji  kwa wale wanaokidhi   vigezo na kukubalika na mamlaka nyengine za uvuvi, na kwamba watapunguziwa gharama za mafuta kwa zaidi ya asilimia 50.

Fursa nyengine kwa wazawa, ni punguzo kwenye gharama za kuingiza vifaa vya uvuvi wa bahari kuu na kwa wanaotaka kuwekeza katika viwanda vya uchakataji mazao ya baharini.

Kuhusu wawekezaji wa ndani kufanya ubia na makampuni ya nje, alisema kunaleta faida kubwa kwa zaidi ya asilimia 90, hatua inayokuza uchumi wa buluu nchini, kukuza ajira katika viwanda vya kuchakata samaki, na pia sekta nyengine zitachochea uvuvi wenye tija.

Alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021, mamlaka imetoa leseni sita za uvuvi wa bahari kuu, ambapo meli tatu kati ya hizo zilitoka nje na tatu nyengine zilikuwa za hapa nchini.

Aliongeza kuwa, katika kipindi hicho, mamlaka ilikusanya shilingi 280,000,000 kutokana na leseni, tofauti na matarajio, kuvuna shilingi bilioni 4.8.

Hata hivyo, alilitaja janga la maradhi ya COVID 19 lililoikumba dunia kuanzia mwishoni mwa mwaka 2019, kuwa ni sababu kuu ya kushuka mapato yaliyokuwa yametarajiwa.

“Janga hili limetuathiri sana kwa kupunguza mapato yatokanayo na usajili wa meli za uvuvi wa bahari kuu kutokana na kizuizi cha kuingia mabaharia na wageni wengine katika nchi mbalimbali duniani,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Alisema ni meli tatu tu kati ya 45 kutoka nje ya nchi zilizojisajili katika mamlaka hiyo, ndizo zilizomudu kuingia nchini, tatizo kubwa likiwa ni ugonjwa wa COVID 19 unaoendelea kuitesa dunia hadi sasa.

Alisema katika awamu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021, mamlaka ikishirikiana kwa karibu na jamii kupitia taasisi ya utafiti ya uvuvi Tanzania, wamefanya tafiti kadhaa za uvuvi.

Dk. Sweke alisema, kwa sasa kuna mikakati ya kufanya utafiti wa bahari kuu ili kubaini aina za rasilimali nyengine zinazopatikana katika uchumi wa buluu wakiwemo samaki wanaoweza kuvuliwa kwa aina nyengine ya uvuvi ili kuongeza uzalishaji zaidi.

Alisema miongoni mwa hatua zilizofikiwa kwa sasa, ni pamoja na kutoa elimu kwa wazawa ili waweze kuona na kutambua maeneo yenye samaki wengi pamoja na matumizi ya kifaa cha JPS kinachosaidia kufika maeneo maalum ya kuvua.

Kifaa hicho kinasaidia pia kuokoa gharama za mafuta na muda pamoja na kuhakikisha usalama wa wavuvi.

Kwa upande mwengine, alisema wamefanya tafiti za uvuvi wa upondo ambao kwa kawaida inatumia meli ndogo, kwa lengo la kuwasaidia wazawa kufika bahari kuu kwa uvuvi endelevu.

Pamoja na tafiti zilizofanyiaka, pia alisema wamewapatia nyezo mbalimbali wazawa na kugaiwa maeneo tofauti.

Aidha mamlaka imegawa simu saba kwa kila wilaya kwa ajili ya kukusanya takwimu ili kutambuwa hali ilivyo, pamoja na mizani tano za kupimia samaki ili kuongeza tija kwa wavuvi wazawa wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Aliyataja maeneo yaliyopatiwa simu kwa ajili ya mawasiliano kwenye maeneo yote ya ukanda wa bahari, kuwa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na kisiwa cha Pemba.

Tanzania bara ni wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Mafia, Tanga, Kilwa na Mtwara, simu zilizotolewa ili kusimamia na kuimarisha rasilimali za uvuvi.

Mkurugenzi huyo alisema elimu zaidi itaendelea kutolewa kwa maofisa uvuvi ikihusisha pia usalama wakiwa baharini, kufanya doria kwa lengo la kudhibiti uvuvi haramu.

Alisema sheria ya bahari ya kimataifa ya mwaka 1982, inatoa maelekezo kwamba ni lazima kuweko mashirikiano ya pamoja na taasisi mahususi inayoshughulikia mambo ya uvuvi, ambayo kwa Tanzania ni DSFA.

Aidha, alisema wanashirikiana na mashirika mbalimbali pamoja na nchi jirani kwa kupeana taarifa, zikiwemo jumuiya za mwambao za Bahari ya Hindi, Kamisheni ya Jodari ya Bahari, jumuiya za nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi, Kamisheni ya Uvuvi ya Bahari ya Hindi na jumuiya nyengine zinazopakana nazo kama vile SADC (Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika).

Alisema Tanzania imewekeza katika uvuvi wa bahari kuu kupitia mashirika ya uvuvi ya ZAFICO kwa Zanzibar na TAFICO upande wa Tanzania Bara.

Mkurugenzi huyo alisema kwa kuwa rasilimali za bahari kuu zina mfumo wa kuhamahama ambapo hutokea msimu samaki wanakuwa wengi hapa Tanzania, kuwepo meli ya kuvulia kutasaidia katika kipindi ambacho hali ya uvuvi baharini inakuwa sio nzuri.

Dk. Sweke alisema mikakati ya mamlaka ni kuimarisha uvuvi wa bahari kuu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari maalum ya uvuvi na viwanda vya kuchakatia samaki.

Mkakati mwengine, alisema ni kuwezesha upatikanaji miundombinu mbalimbali ikiwemo majokofu kwa ajili ya kuhifadhia samaki sambamba na kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji wa ndani na nje kupitia uchumi wa buluu.

Kuhusu mamlaka kutoa leseni ya uvuvi wa samaki aina ya jodari na jamii zake, alisema hiyo haimaanishi kuwa katika bahari kuu kuna aina hiyo tu ya samaki bali wapo wa aina nyengine tena wengi.

Alibainisha jodari anapendwa sana katika nchi zilizoendelea hasa Japan na Marekani ambako soko lake huko ni kubwa, lakini kuna aina nyengine za samaki wanaoweza kuvuliwa na kuuzwa katika masoko yetu ya ndani na kupunguza upungufu wa upatikanaji wa mazao ya uvuvi nchini, ikizingatiwa Tanzania inazalisha nusu ya mahitaji ya samaki.

Alisema kama mamlaka itafanya tafiti ili kuona maeneo yenye samaki wengi wakiwemo vibua na wengine, kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza uvuvi na kutosheleza mahitaji ya samani kwa kuacha kuagiza kitoweo kutoka nje.

Alitoa wito kwa wazawa kuwekeza katika miundombinu inayojumuisha mnyororo wa thamani wa uvuvi wa bahari kuu ili kuingiza fedha za kigeni kwa taifa wao kupata faida itokanayo na kazi ya mikono yao.

Halikadhalika, alisema kufanya hivyo, kutaongeza nafasi za ajira kwa Watanzania kupitia sekta ya uvuvi ambayo kimsingi ni eneo lenye utajiri mwingi endapo litapewa kipaumbele na kufanyiwa kazi kitaalamu.

Mwandishi wa makala haya pia alizungumza kwa muhtasari na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) Dk. Ameir Haidar Mshenga, ambaye aliwashauri wazawa kuwa na tabia ya kuingia kwenye mitandao kufuatilia taarifa zinazohusiana na uchumi wa buluu kupitia bahari kuu.

Alisema kwa sasa, ZAFICO imenunua meli moja iliyopewa jija la ‘SEHEWA TWO’ ambayo inafanya kazi katika bahari kuu.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kuongeza meli nyengine itakayoitwa ‘SEHEWA THREE’ ikiazimia kuleta mabadiliko katika uchumi wa buluu kwa kuvua samaki wakubwa katika maji ya kina kikubwa.

Dk. Mshenga alisema kutokana na wazawa kutokuwa na uzoefu kwenye uvuvi wa bahari kuu, Shirika hilo limetoa mafunzo maalum kwao juu ya kuendesha uvuvi wa biashara katika bahari kuu.

Alisema mafunzo hayo yametolewa kwa mikupuo sita ya wavuvi waliofanya mazoezi katika meli ya ‘SEHEWA TWO’.

Aliwaasa vijana wa Zanzibar waache kuukalia uchumi walionao, na kuwataka wachangamke kuusaka utajiri uliosheheni kwenye rasilimali ya bahari ambayo Mwenyezi Mungu amevijaalia visiwa vya Unguja na Pemba.