NA MWAJUMA JUMA
DAKTARI dhamana wa wilaya ya Mjini Unguja, Ramadhan Mikidadi amesema bado kuna mwamko mdogo wa wananchi kwenda vituoni kupata chanjo ya UVICO 19.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mikidadi alisema mpaka sasa wimbi kubwa la watu wanaokwenda kupata chanjo ni wafanyakazi wa taasisi za serikali, wazee kuanzia umri wa miaka 55 na kuendelea na wasafiri.
Alisema hali hiyo inatokana na woga pamoja na kutawaliwa na mitazamo hasi juu ya suala zima la chanjo hiyo. “Bado mwamko ni mdogo na woga ndio unaowafanya wananchi wa kawaida kuja unaoendana mitazamo hasi na chanjo hiyo”, alisema.
Hata hivyo alisema pamoja na changamoto hiyo wamekuwa wakiendelea na kazi ya uhamasishaji kupitia kitengo cha kutoa elimu ya afya cha wizara pamoja na wilaya yao.
Alieleza kwamba mpaka sasa wilaya ya mjini mpaka sasa wana vituo viwili vinavyotoa chanjo kikiwemo cha Hospitali ya Rahaleo na Mpendae.
Aidha alisema wanampango wa kuongeza vituo vyengine viwili Polisi Ziwani na Kwamtipura.
Hata hivyo alisema katika kituo cha Rahaleo kwa siku wanapokea watu zaidi ya 100 ambao hufika kupatiwa chanjo hiyo.
Sambamba na hayo aliwataka wananchi kuacha mitazamo hasi juu ya chanjo hiyo na chanjo hiyo ni salama na kuchanja kwa chanjo hicho kunapunguza vifo vitokanavyo na maradhi hayo.
Kwa upande wake ofisa Afya Jamii wa Wizara ya Afya, Yahya Mbwana Mselem alisema changamoto ambayo ipo kwa sasa ni wale ambao waliochanja kutokufika kuchukuwa kadi zao.
Alisema Zanzibar kuna chanjo za aina tatu ambazo wanachanja ikiwemo ya Jonson Jonson, Sinovac na Sputnick Light na tokea kuanza chanjo hiyo watu karibu 20,000 wamechanja, ambapo lengo lao ni kupata watu milioni moja.