NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza dhana ya uchumi jumuishi kwa vitendo kwa kuweka vipaumbele vitakavyowawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Alisema hayo jana kwenye ufunguzi wa kongamano la tano la uwezeshaji wananchi Kiuchumi, jijini Dodoma, ambapo alibainisha kuwa vipaumbele katika mipango ya serikali vimekuwa katika utekelezaji wa shughuli za kiuchumi zinazowajumuisha wananchi.

Majaliwa alitaja baadhi ya vipaumbele hivyo ni pamoja na uimarishaji wa huduma za afya, hifadhi ya jamii, maji, umeme na utekelezaji wa mpango wa elimu msingi bila ada “Mtanzania mwenye afya, aliyeelimika na miundombinu wezeshi ni chachu kwa ukuaji uchumi wa nchi yetu.”

Alisema uwezeshaji wa uchumi jumuishi ni msingi wa kuhakikisha kunakuwa na ustawi endelevu kwa watu wote, ambapo serikali imeandaa dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025 ambayo imeainisha mazingira wezeshi yatakayofanikisha nchi kunufaika kiuchumi.

Alisema dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025 pia imelenga kuhakikisha kunakuwa na viwango vya juu vya maisha, amani na umoja, utawala bora na uchumi ulioimarika wenye ushindani katika jamii.

Aidha Majaliwa alisema serikali imeandaa sera zilizolenga kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu na uchumi jumuishi, ikiwemo sera ya Taifa ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004.

Kadhalika, waziri mkuu ametumia fursa hiyo kutoa maagizo kwa viongozi wa wizara, mikoa, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa masuala ya uwezeshaji wahakikishe dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuiwezesha nchi kuwa na uchumi jumuishi itimie.

Aliongeza kuwa viongozi wa mikoa wasimamie uimarishwaji wa majukwaa ya wanawake kwenye mikoa kama ilivyoelekezwa na Rais Samia alipokutana na wanawake jijini Dodoma Juni 8 mwaka huu.

Wakati huo huo, waziri mkuu alizindua kanzidata ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo ipo chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikiwa na lengo la kuwaunganisha watoa huduma wa kitanzania na wawekezaji pamoja na taasisi mbalimbali za uwezeshaji.

Kwa upande wake, waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geoffrey Mwambe aliwaagiza wakuu wa mikoa wasimamie shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi katika maeneo yao na zinakuwa na tija ili kuhakikisha malengo ya Mheshimiwa Rais Samia yanafikiwa.

Waziri Mwambe alisema kwamba kongamano la uwezeshaji wananchi kiuchumi lilianzishwa mwaka 2015/2016 ili kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji kwa lengo la kujadili na kupeana uzoefu katika kuwawezesha watanzania.