NA LAYLAT KHALFAN

MKURUGENZI wa Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Abdallah Saleh Omar, ameitaka jamii kuhakikisha inatekeleza jukumu la kuwatunza wazee kwa kuwapatia haki zote zinazostahiki.

Aliyaeleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika ukumbi wa Kidongo chekundu, wenye lengo la kuongeza uwelewa juu ya masuala yanayowahusu wazee na wajibu wao katika kusukuma utekelezaji wake.

Alisema wazee wengi katika baadhi ya familia wanadharaulika kwa kutoonekana thamani yao huku wengine wakikabiliwa na manyanyaso yakiwemo yanayofikia uvunjifu wa amani.

Alisema ili kuwa na jamii yenye ustawi mzuri na maendeleo endelevu kwa kila mtu ana kila sababu ya kuweka mikakati endelevu inayozingatia usawa wa kijinsia na mahitaji ya kila rika hususan wazee kwa kuwa wao tayari wamepoteza nguvu.

Aidha, Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa, miongoni mwa mikakati hiyo ni kushajihisha uanzishwaji wa mfumo wa kisheria ili kulinda wazee walio katika hali hatarishi dhidi ya udhalilishaji.

Sambamba na hayo aliisisitiza jamii kuchukua jitihada za makusudi katika kuunganisha nguvu za pamoja katika kumtunza mzee, ambapo katika ujana wao wametumia nguvu kujenga familia na walikuwa tegemeo la uzalishaji nchini.

Naye Meneja Miradi Kinga jamii kutoka HelpAge International, Jerome Mwaya alisema wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kipato duni, udhaifu wa huduma za afya mambo ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi.

Aidha, Mwaya alisema kutokana na hali hiyo ipo haja ya kutumia fursa ya kuwaimarishia maisha mazuri wazee kwa maslahi yao na wao pindi wakifikia uzeeni waweze kunufaika.

Akiwasilisha mada kuhusiana na mabadiliko yanayotokea kwa wazee, Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii, Selwa Ali Sheha alisema wazee wengi hukabiliwa na kinga pungufu kwenye miili yao na kukosa nguvu za mwili kutokana na kuchoka viungo na kusababisha kupungua kipato chao cha kila siku.

Hivyo ipo haja ya kusaidiwa, kutunzwa na kuthaminiwa kwa lengo la kujipatia kipato cha uhakika kukidhi mahitaji yao kwa kuwekewa ajenda makhsusi kwa lengo la kuinuliwa katika kipato.