LILONGWE, MALAWI

NAIBU Spika wa bunge wa zamani wa Malawi amejiuwa kwa kujipiga risasi kichwani ndani ya bunge ambako alikwenda kwa ajili ya mkutano.

Clement Chiwaya aliyekuwa na umri wa miaka 50 alijiuwa akiwa ndani ya majengo ya bunge ambapo ilielezwa kuwa alikwenda kwa lengo la kujadili mafao ya gari aliyopewa wakati alipoacha wadhifa huo mwaka 2019.

James Kadadzera msemaji wa polisi ya Malawi alithibitisha tukio hilo la mauaji lakini amekataa kutoa maelezo hadi atakapopokea taarifa kamili ya uchunguzi.

Taarifa ya bunge la Malawi ilieleza kuwa inasikitishwa kuutarifu umma kwamba Naibu Spika wa zamani wa bunge la nchi hiyo amejiuwa akiwa katika majengo ya bunge.

Iliongeza kuwa mauaji hayo yanahusishwa hali ya kuchanganyikiwa na usumbufu uliokuwa ukimkabili kufuatia kushindwa kutekelezewa malipo ya hasara na mafao yake.

Bunge la Malawi lilieleza kuwa, Chiwaya alijiua kwa kujipiga risasi kichwani akiwa ndani ya ofisi ya karani wa bunge Fiona Kalembera.

Kabla ya kuwa Naibu Spika Clement Chiwaya alikuwa mbunge kuanzia mwaka 2004.

Ilielezwa kuwa Chiwaya alinunua gari yake rasmi mwaka 2019 mwishoni mwa kumalizika muhula wake wa utumishi kwa mujibu wa mkataba wa kazi.

Lakini alikuwa akijaribu kulitaka bunge lilipe gharama za uharibu kufuatia ajali ya gari aliyopata miezi sita baadaye hata hivyo jitihada zake ziliambulia patupu.

Aidha alifungua kesi mahakamani na hadi anajiuwa mchakato wa kisheria ulikuwa ukisubiriwa.