LONDON, England

CRISTIANO Ronaldo  mshambuliaji wa klabu ya Manchester United, alifunga bao la ushindi katika dakika za lala salama, wakati Manchester United ikiitungua mabao 2-1 Villarreal katika mchezo wa ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbele ya mashabiki 73,130 waliohudhuria Uwanja wa Old Trafford Ronaldo alivunja rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi za ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa amefanya hivyo mara 178 na bao lake la dakika ya 90+5 likiipa pointi United katika kundi F.

Ni Paco Alcacer alianza kufunga dakika ya 53 ila lilisawazishwa  na Alex Telles kisha bao la ushindi likawekwa kimiani na Ronaldo ambaye aliivunja rekodi ya Iker Casillas aliyekuwa anashikilia rekodi ya kuwa nyota ambaye amecheza mechi nyingi za ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kucheza mechi 177 huku mshikaji wake Lionel Messi ambaye yupo PSG amecheza mechi 151 akiwa ni namba tatu.

Mchezo mwengine Benfica wamewatandika Barcelona mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi E ligi ya Mabingwa Ulaya Uwanja wa Luz Jijini Lisbon, Ureno.

Mabao ya Benfica yamefungwa na Darwin Núñez dakika ya tatu na 79  kwa penalti na Rafa Silva dakika ya 69 na kwa kipigo hicho cha pili mfululizo, Barcelona inashika mkia nyuma ya Dinamo Kiev yenye pointi moja.

Bayern Munich wanaongoza sasa kwa pointi zao sita, wakifuatiwa na Benfica yenye pointi nne.

Wenyeji Juventus wameutumia vizuri Uwanja wa nyumbani, Allianz Jijini Torino, baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Chelsea katika mchezo wa Kundi  H bao pekee la Federico Chiesa dakika ya 46.

Ushindi huo unawapandisha kileleni Juve wakifikisha pointi sita,     wakati  Chelsea inabaki na pointi zake tatu sawa na Zenit, huku Malmö ambayo haina pointi ikiwa inashika mkia.