NA SAIDA ISSA, DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali nchini kuongeza uwazi, uwajibikaji, kwenda sambamba na vipaumbele na mipango ya serikali ili ziweze kuleta tija katika jamii.

Samia alisema hayo jana wakati akihutubia katika mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete kijini Dodoma.

Rais Samia alisema kwa sasa serikali inatekeleza mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano (2021/2026) hivyo ni vyema mashirika hayo kuandaa mipango yake kwa kuoanisha na mpango huo wa serikali.

Aidha aliyataka mashirika hayo hayo hususan ya ndani pamoja na wizara husika kuandaa mpango mkakati utakaosaidia kuondokana na utegemezi katika utendaji wa kazi zao.

“Mimi ni zao la mashirika yasiyo ya kiserikali kwa miaka10 nlikuwa nikifanya kazi kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali ndio maana hata nilipopata mualiko huu sikusita kuja nikijua mimi ni mwenzenu”, alisema.

Alisema Samia alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaendelea kuboresha mazingira ili kuimarisha utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali hapa nchini.

Ambapo alisema jumla ya mashirika yaliyosajiliwa Tanzania bara na Zanzibar ni 11,603, yanayofanya kazi ni 4,663.

“Mwaka 2001 Serikali ilitunga sera na Sheria kwa ajili ya mashirika yasiyo ya kiserikali na mwaka 2005/09 Serikali ilifanya marekebisho lengo ikiwa ni kiyawezesha mashirika haya kufanyakazi katika mazingira mazuri”, alisema.