NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema wadau wa vyama ushirika wanamchango mkubwa katika kuimarisha Uchumi na  kusaidia kasi ya maendeleo katika jamii.

Akizungumza na kamati ya maandalizi ya siku ya ushirika duniani wakati akipokea ripoti ya utekelezaji  baada ya kumalizika  maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika  mwezi Julai mwaka huu.

Alisema kufanyika kwa sherehe hizo kutasaidia kushajihisha na wanaushirika wengine kujiunga na vyama hivyo ambapo itapelekea kujitangaza pamoja na kuinuka kiuchumi.

Alisema makongamano hayo ni muhimu na ni vyema kuendelea kuwepo pamoja na kukutana, ili kuona vyama hivyo vinaingia kwa pamoja.

“Ni jambo zuri kwani litasaidia hata kuwepo kwa vyama vingi ambavyo vitakuwa na msongamano na kutofikia lengo lilokusudiwa, hivyo nawapongeza kwa kuundwa kwa vyama hivi” alisema.

Aidha alisema siku ya ushirika duniani ni muhimu kwani itawasaidia wanaushirika kuwapa mashirikiano kwa kuleta mafanikio zaidi duniani.

Sambamba na hayo, aliitaka kamati hiyo kaangalia kasoro zinazojitokeza katika kuandaa sherehe hizo, ili shughuli zilizopangwa kwa siku hiyo zitekekelezwe kwa wakati na kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Ushirika, Khamis Daudi Simba, alisema, kamati hiyo iko tayari kufuata muongozo na maelekezo aliyoyatoa Waziri, ili kuendeleza utekelezaji wa shughuli za ushirika .

“Miongozo uliyotupa ni mizuri na sisi tutaitahidi kuitekeleza penye masuala tutakufata ili uweze kutushauri zaidi” alisema.